Oct 15, 2021 06:36 UTC
  • Iran yaonya kuhusu hatari ya kimya cha IAEA mbele ya silaha za atomiki ya Israel

Balozi na mjumbe maalumu wa Iran katika Taasisi za Kimataifa zenye makao yao mjni Vienna Austria amekosoa vikali kimya cha Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA mbele ya mradi wa silaha za atomiki za Israel na kusema kuwa, undumilakuwili wa taasisi hiyo ya kimataifa unachochea uzalishaji wa silaha hizo angamizi duniani.

Balozi Kazem Gharib Abadi amesema hayo kupitia ukurasa wake wa Twitter na kuhoji kwa kusema, ni nini faida ya kuwa mwanachama wa Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Atomiki NPT? Kuna faida gani kwa IAEA kushikiliza utekelezaji kamili wa vipengee vya taasisi hiyo wakati yenyewe inanyamazia kimya utengenezaji wa silaha hizo unaofanywa na baadhi ya madola kama utawala wa Kizayuni wa Israel? 

Amesema, kunyamazia kimya na kudharau uundaji wa silaha za nyuklia unaofanywa na Israel kuna ujumbe hasi kwa wanachama wa NPT na kunawafanya waamini kuwa hakuna tofauti yoyote baina ya kuwa mwanachana au kutokuwa mwanachama wa mkataba huo wa kuzuia uzalishaji na uenezaji wa silaha angamizi za nyuklia duniani.

Balozi Kazem Gharib Abadi

 

Katika mahojiano aliyofanyiwa hivi karibuni na tovuti ya Energy Intelligence na wakati alipoulizwa swali kwa nini anazungumzia mno mradi wa nyuklia wa Iran na kuacha kabisa miradi ya madola mengine hasa wa Israel, Rafael Grossi, Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA alijibu kiurahisi tu kwamba ni kwa sababu Israel si mwanachama wa Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Atomiki (NPT), na hata haijatia saini mkataba huo wakati Iran ni mwanachama. 

Iran inasema, kama hakuna hatua zozote za maana zinazochukuliwa na NPT, kuna faida gani ya kuwa mwanachama wa mkataba huo? 

Hivi sasa inakadiriwa kuwa utawala wa Kizayuni wa Israel unamiliki karibu vichwa 300 vya silaha angamizi za nyuklia, na hakuchukuliwi hatua yoyote dhidi yake.