Oct 19, 2021 00:45 UTC
  • Iran yaitaka OIC ilaani mashambulio ya kigaidi ya ISIS nchini Afghanistan

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa lengo la genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh (ISIS) huko Afghanistan ni kuchochea chuki na uadui wa kimadhehebu na ameitaka Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC ilaani vikali vitendo vya kinyama vya Daesh.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo katika mazungumzo yake ya simu na Katibu Mkuu wa OIC, Yousef  al Othaimeen na kusisitiza kuwa magenge yenye misimamo mikali ya kigaidi ndio mgogoro mkubwa katika Uliwengu wa Kiislamu leo hii. Amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono kikamilifu nafasi amilifu ya OIC katika utatuzi wa mgogoro wa Afghanistan hasa kwenye kupambana na hali mbaya ya hivi sasa ya vitendo vya kigaidi vya Daesh.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amegusia pia jinai za hivi karibuni za magaidi wa ISIS za kuwashambulia kinyama na kikatili Waislamu waliokuwa wanasali misikitini huko Kunduz na Kandahar nchini Afghanistan na kusisitiza kuwa, OIC na wanachama wote wa jumuiya hiyo pamoja na Katibu Mkuu wake, wanapaswa kulaani ukatili na unyama huo wa Daesh.

Magaidi wanafanya jinai kubwa dhidi ya Waislamu wa Afghanistan tena ndani ya Misikiti

 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC amesema kuwa, inabidi serikali mpya ya Afghanistan ijumuishe watu wa makundi na matabaka yote, ichunge haki za binadamu zikiwemo za wanawake, ilete mshikamano baina ya Waafghani na ihakikishe Afghanistan haigeuki kuwa chaka la amani kwa magenge ya kigaidi.

Yousef  al Othaimeen amegusia pia mazungumzo yanayoendelea baina ya Iran na Saudi Arabia na juhudi za kufunguliwa ofisi ya mwakilishi wa Iran ndani ya OIC huko Jiddah Saudi Arabia akisema kuwa, ana matumaini mazungumzo baina ya Tehran na Riyadh yatazaa matunda mazuri.

Tags