Oct 20, 2021 02:21 UTC
  • Sisitizo la Iran la Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kuwa na mchango amilifu zaidi nchini Afghanistan

Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, lengo la genge la kigaidi na ukufurishaji la Daesh huko Afghanistan ni kuchochea chuki na uadui wa kimadhehebu na ameitaka Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC ilaani vikali vitendo vya kinyama vya Daesh.

Amir-Abdollahian amesema hayo katika mazungumzo yake ya simu na Yousef Al-Othaimeen, Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na kusisitiza kuwa, wanachama wote wa jumuiya hiyo pamoja na Katibu Mkuu wake, wanapaswa kulaani ukatili na unyama huo wa Daesh ulio dhidi ya utu na ubinadamu.  Amesema, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaunga mkono kikamilifu nafasi amilifu ya OIC katika utatuzi wa mgogoro wa Afghanistan hasa kwenye kupambana na hali mbaya ya hivi sasa ya vitendo vya kigaidi vya Daesh.

Wananchi wa Afghanistan kwa zaidi ya miongo miwili wamekuwa wahanga wa hatua za kupenda vita za Marekani na hivi sasa pia wamekuwa walengwa wa jinai za kundi la kigaidi la Daesh ambalo limepenya na kuingia nchini Afghanistan kwa himaya na uungaji mkono wa Marekani. Katika kipindi cha miezi michache ya hivi karibuni, kundi la kigaidi la Daesh likiwa na lengo la kuzusha fitina na mifarakano baina ya Waislamu wa Kishia na Kisuni, limekuwa likiilenga kwa hujuma za kigaidi Misikiti ya Waislamu wa madhehebu ya Shia nchini Afghanistan.

Takribani waumini 40 waliokuwa katika ibada ya Swala ya Ijumaa waliuawa shahidi na wengine karibu ya mia moja walijeruhiwa katika milipuko miwili iliyotokea Ijumaa iliyopita katika Msikiti wa Bibi Fatima katika mji wa Qandahar Afghanistan. Kundi la kigaidi la Daesh lilitangaza kuhusika na jinai hiyo.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC)

 

Hilo lilikuwa shambulio la kigaidi la mara kadhaa lililotokea nchini Afghanistan. Shambulio la kwanza la kigaidi nchini Afghanistan lilitokea jirani na uwanja wa ndege wa Kabul wiki ya pili tu baada ya wanamgambo wa Taliban kushika hatamu za nchi hiyo. Kundi la kigaidi la Daesh tawi la Khorasan lilitangaza kuhusika na hujuma hiyo ambayo ilipelekea takribani watu 200 kuuawa wakiwemo watoto na wanawake. Wiki chache zilizopita  pia kulitokea mlipuko jirani na Msikiti wa Eid Gah mjini Kabul ambapo kwa akali watu wanane waliuawa na wengine 20 kujeruhiwa.

Operesheni ya kigaidi katika msikiti wa Qandahar ilitekelezwa baada ya kutokea mlipuko mwingine katika msikiti wa Sayedabad huko Kunduz ambapo watu wasiopungua 60 waliuawa  shahidi. Misikiti yote hiyo ni ya Waislamu wa madhehebu ya Shia. Kundi la kigaidi la Daesh lilitangaza pia kwamba, ndilo lililohusika na hujuma na jinai hizo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali jinai hizi na imeonyesha wasiwasi ilionao wa kuendelea matukio na jinai kama hizi huko nchini Afghanistan. Kushindwa serikali ya muda ya Afghanistan inayoongozwa na Taliban kukabiliana na hujuma na mashambulio haya ya kigaidi ya Daesh na kuendelea jinai katika nchi hiyo ni tatizo kuu na la kimsingi ambalo utatuzi wake unahitajia hatua za maana na madhubuti.

 

Wanachama wa Daesh nchini Afghanistan

 

Suala jingine muhimu ni majukumu ya Ulimwengu wa Kiislamu pamoja na nchi wanachama wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC).  Nchi za Kiislamu licha ya uwezo zilizonao, hazijachukua hatua athirifu kwa ajili ya kukabiliana na ugaidi na kundi la kigaidi la Daesh. Afghanistan ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Marekani kuanzia mwaka 2001 na ni miezi michache tu iliyopita ambapo Washington imeondoa majeshi yake katika nchi hiyo. Katika kipindi chote hicho, wananchi wa Afghanistan walikuwa wahanga wa uwepo huo na chokochoko za ikulu ya White House pamoja na majeshi ya NATO.

Katika kipindi chote hiki, jumuiya na asasi za haki za binadamu duniani ziliamua kunyamaza kimya na kutosema chochote kuhusiana na jinai za Marekani na washirika wake nchini Afghanistan. Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) nayo ambayo kimsingi ilipasa kuwa tegemeo na mtetezi wa haki za Waislamu, imeshindwa kabisa kutekekeza ipasavyo majukumuu yake na badala yake imekumbwa na maradhi ya kigugumizi katika uchukuaji maamuzi.

Filihali, hali ya wananchi wa Afghanistan inatia wasiwasi mno na kunahisika  haja kubwa ya kudhaminiwa usalama kwa mirengo na makundi yote ya kisiasa, kikaumu na kimadhehebu. Hapana shaka kuwa, endapo hakutaandaliwa mipango na mikakati imara kwa ajili ya kuimarisha usalama na wakati huo huo kukaendelea kushuhudiwa hali ya kutokuwa na uwezo wa kukabiliana na ugaidi, mgogoro wa Afghanistan utaingia katika hatua na marhala nyingine. Katika wakati huu mgumu, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko pamoja na wananchi wa Afghanistan na iko tayari kutoa msaada wa aina yoyote na wa kila upande, kwa minajili ya kurejesha amani na uthabiti wa kudumu katika nchi hiyo.

Shambulio la kigaidi la msikiti wa Mashia katika mji wa Kunduz Afghanistan

 

Kuhusiana na hilo, Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran juzi Jumatatu alifanya mazungumzo pia na Antonio Guterres, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ambapo sanjari na kueleza wasiwasi wa Tehran kuhusiana na hali ya Afghanistan alimtaka Katibu Mkuu huyo achukue hatua za maana katika kusimamisha na kukabiliana na ugaidi nchini Afghanistan.

Mazungumzo ya Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na maafisa wa Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) na sisitizo la kuwa na mchango na nafasi muhimu zaidi asasi za kimataifa na nchi za Kiislamu kuhusiana na matukio ya Afghanistan, yanakumbusha umuhimu wa suala hili kieneo na kimataifa.

Tags