Oct 21, 2021 02:21 UTC
  • Mkutano wa 35 wa Umoja wa Kiislamu, mwelekeo na malengo

Mkutano wa 35 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ulianza Jumanne ya wiki hii mjini Tehran kwa hotuba ya Rais Sayyid Ebrahim Raisi ukijadili maudhui ya umoja wa Kiislamu, amani na kujiepusha na mifarakano na mizozo katika Ulimwengu wa Kiislamu. Mkutano huo ni sehemu ya sherehe za Maulidi na kumbukumbu ya kuzaliwa mbora wa viumbe na Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw).

Mkutano huo unashirikisha wasomi na wanafikra wa Kiislamu kutoka zaidi ya nchi 51 duniani.

Katika sehemu moja ya hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo, Rais Ebrahim Raisi amesema kuwa mkutano huo una nafasi na mchango muhimu na wa kistratijia katika kuzindua Umma wa Kiislamu mkabala wa njama nyingi zinazoukabili. Sayyid Raisi ameashiria jinsi kundi la Daesh linavyohudumia malengo ya Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel na kusema: Njama hiyo inashuhudiwa vyema hii leo huko Lebanon na Afghanistan kama ilivyoshuhudiwa jana huko Iraq na Syria. Hivyo kuna umuhimu mkubwa wa kutambua vyema njama hiyo na hapana shaka kuwa, juhudi za wanazuoni na wasomi wa Kiislamu za kuweka wazi na kufichua njama hiyo zinaweza kuwalinda vijana katika Umma wa Kiislamu.

Kwa sasa nchi za Kiislamu zinakabiliwa na vitisho na changamoto nyingi, na muhimu zaidi ni zile za kutaka kuzusha hitilafu, mizozo ya kikanda na kuimarisha harakati za ugaidi. Changamoto hizo kwa hakika ni tishio kwa mustakbali wa nchi zote za Magharibi mwa Asia na Ulimwengu wa Kiislamu kwa ujumla. Ugaidi na misimamo ya kuchupa mipaka si tishio kwa nchi za Iraq na Syria pekee bali ni hatari pia kwa usalama na amani ya kimataifa. Hali inayotia wasiwasi na harakati za magaidi wa Daesh huko Afghanistan ni ushahidi wa wazi wa ukweli huo. Hivyo basi, kupambana na njama za kuzusha mifarakano na makundi yanayofanya mikakati ya kuvuruga amani na mshikamano na kuzusha migawanyiko kuna umuhimu wa kistratijia. 

Hata hivyo suala la kuwepo umoja na mshikamano katika Umma wa Kiislamu linahitajia juhudi za kuweka wazi njama zinazofanywa na maadui na mabeberu wa kimataifa kama Marekani na kuimarisha sababu za umoja katika mataifa ya Waislamu. 

Marekani daima haitaki kuona amani na usalama ukitawala katika nchi za Waislamu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, kulinda usalama na uwepo wa dola bandia na haramu la Israel na maslahi ya madola ya kibeberu kunawezekana kupitia njia ya kuudhofisha Umma na mataifa ya Waislamu. Hivyo, maadui hao hususan Marekani, daima hufanya njama na mikakati ya kudhoofisha Umma na nchi za Kiislamu na kuzifanya tegemezi kwa madola ya kigeni. Wanasiasa wa Marekani wanasisitiza kuwa, kuna ulazima wa kulitumbukiza eneo la Asia Magharibi katika vita na mapigano ili kuhakikisha kwamba, utawala wa Israel unapata amani na usalama.

Emad Hamron ambaye ni mhadhiri wa chuo kikuu na mchambuzi wa masuala ya siasa wa Ufaransa amesema katika kikao cha kwanza cha Mkutano wa 35 wa Umoja wa Kiislamu unaofanyika mjini Tehran kwamba: Hii leo Palestina na baadhi ya maeneo ya Syria yanakaliwa kwa mabavu, na kunashuhudiwa vita na mapigano katika maeneo kadhaa ya Waislamu kutokana na njama inayotekelezwa kwa kutumia makundi ya kitakfiri. Hali hii ina maana ya kufeli na kushindwa wanafikra wa Ulimwengu wa Kiislamu, wasomi na wanasiasa wa Umma katika jitihada za kuimarisha umoja na udungu.

Mchambuzi huo wa Kifaransa ameongeza kuwa: “Inasikitisha kuwa, ukoloni umeweza kutumia mifarakano na hitilafu zilizojitokeza katika historia yetu. Hivyo kuna udharura wa kufuta na kuondoa athari mbaya za hitoiafu na mifarakano hiyo.”

Viongozi wa serikali ya Marekani daima wamekuwa wakifanya jitihada za kuzusha hitilafu na hali ya kutoaminiana katika uhusiano wa Iran na nchi za Asia Magharibi kupitia njia ya kutoa tuhuma zisizo na msingi. Haya yanafanyika kwa shabaha ya kuipatia Marekani na vibaraka wake katika eneo hilo fursa nzuri zaidi ya kutekeleza njama na mipango yao ya kishetani. Hata hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesimama imara mbele ya njama hizo za madola ya kibeberu na daima imekuwa ikitilia mkazo udharura wa kuwepo umoja na mshikamano baina ya mataifa yanayokandamizwa; suala ambalo linazidi kuikasirisha serikali ya Washington na utawala wa Kizayuni wa Israel.

Tunamalizia kwa kusisiza kuwa Uislamu ni dini ya umoja na mshikamano na unapinga mifarakano, mizozo, mapigano baina ya wanadamu na fikra mgando za kuchupa mipaka na unasisitiza kuwa umoja na maelewano ndiyo njia ya kujiondoa katika matatizo ya aina mbalimbali na kuepuka njama na mipango ya maadui wa mwanadamu.