Oct 21, 2021 07:58 UTC
  • Raisi Ebrahim Raisi: Stratijia ya Iran ni kuwepo umoja baina ya Waislamu

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, stratijia ya Iran ni kuhakikisha kwamba kunakuwepo umoja na mshikamano katika Ulimwengu wa Kiislamu.

Sayyid Ebrahim Raisi aliyasema hayo jioni ya jana mjini Tehran katika kikao cha baraza la mawaziri. Amewapongeza Waislamu wote duniani kwa mnasaba wa siku hizi za kusherehekea Maulidi na kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (saw) na mjukuu wake, Imam J'afar Swadiq (as) na vilevile kuanza wiki ya umoja baina ya Waislamu na kusema: Umoja baina ya Waislamu ni stratijia ya Iran, ilhahi stratijia ya maadui wa Umma ni kuhakikisha kunakuwepo hitilafu na mifarakano katika Ulimwengu wa Kiislamu. 

Rais Ebrahim Raisi ameongeza kuwa, Mtume Muhammad (saw) na Ahlubaiti wake watoharifu ndiyo nembo ya umoja na mshikamano baina ya Waislamu na jami ya wanadamu kwa ujumla na kusema: Kila mtu anayetenda kinyume na umoja na mshikamano baina ya Waislamu anahudumia maslahi ya maadui wa Umma wa Kiislamu. 

Vilevile ametilia mkazo udharura wa kuimarishwa umoja na mshikamano baina ya makundi, kaumu na jamii zote za Waislamu. 

Jumanne iliyopita wakati akifungua Mkutano wa 35 wa Kmataifa wa Umoja wa Kiislamu unaofanyika hapa mjini Tehran, Rais Ebrahim Raisi pia alisema: Wazo la kuzikurubisha pamoja madhehebu za Kiislamu lililobuniwa na Imam Ruhullah Khomeini (MA), Mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni hatua ya kistratajia katika ulimwengu wa Kiislamu.

Sayyid Raisi alieleza kuwa, mfumo unaotawala dunia hautaki kuona umma wa Kiislamu ukiungana, na hivi sasa, baada ya Vita vya Pili vya Dunia, wanautazama Uislamu kama kizingiti cha kufikia malengo yao.

Mkutano wa 35 wa Kimataifa wa Umoja wa Kiislamu ulianza Jumanne wik hii hapa mjini Tehran kwa mnasaba wa kuanza Wiki ya Umoja na maadhimisho ya Maulidi ya Mtume Muhammad (saw) , chini ya kaulimbiu ya "Umoja wa Kiislamu; Amani na Kuepukana na Mifarakano."       

Tags