Oct 21, 2021 11:28 UTC
  • Iran yaanza mazoezi makubwa ya kijeshi angani

Kikosi cha Anga cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kimeanza mazoezi makubwa yaliyopewa jina la 'Duru ya 10 Uwezo wa Anga wa Waliojitolea Kulinda Anga ya Wilayat'. Mazoezi hayo yamezinduliwa rasmi kwa kutamkwa ' Ya Muhammad Rasulullah SAW.

Kwa mujibu wa taarifa, mazoezi hayo ambayo yameanza leo yanashirikisha vituo vya ndege za kijeshi katika maeneo mbali mbali ya Iran.

Akizungumza na waandishi habari, Naibu Kamanda wa Kikosi cha Jeshi la Anga la Iran Mehdi Hadian amesema mazoezi hayo yatafanyika katika eneo kubwa la Iran.

Ameongeza kuwa, moja ya malengo ya luteka hiyo ni kuweza kubainisha uwezo wa kivita wa kikosi hicho katika mazingira halisi ya kivita.

Naibu Kamanda wa Kikosi cha Anga cha Jeshi la Iran amesema katika mazoezi hayo  makubwa kunatumika zana na silaha ambazo zimeundwa katika viwanda vya Wizara ya Ulinzi ya Iran. 

Mazoezi ya kikosi cha Jeshi la Anga la Iran

Iran hufanya mazoezi makubwa ya kijeshi mara kwa mara ili kubaini uwezo na utayarifu wa vikosi vya ulinzi.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa uwezo wake mkubwa wa kijeshi sio tishio kwa nchi yoyote na kwamba sera zake za ulinzi ni kwa ajili ya kukabiliana na maadui wa nchi hii.