Oct 21, 2021 11:33 UTC
  • Iran yatoa huduma za kitiba kwa waliojeruhiwa katika mlipuko msikitini Afghanistan

Raia wa Afghanistan ambao walijeruhiwa katika hujuma ya kigaidi dhidi ya msikiti Ijumaa katika mji wa Kandahar wamefikishwa mjini Tehran kwa ajili ya matibabu.

Kwa mujibu wa taarifa, majeruhi hao wamesafirishwa kwa ndege kutoka Kandahar hadi Tehran kwa sababu hakuna huduma za kutosha za afya nchini Afghansitan.

Raia hao wa Afghanistan wamelazwa katika Hospitali ya Baqiyatullah hapa mjini Tehran. Mkurugenzi wa hospitali hiyo Dkt. Hasan Abulqasemi amesema baadhi ya majeruhi wanahitaji upasuaji na kuongezwa damu kutokana na majeraha mabaya waliyopata. Aidha amesema miongoni mwa majeruhi kuna watoto kadhaa wadogo ambao nao wamepata matibabu na hali yao inaboroka.

Dkt. Abulqasemi amesema hospitali hiyo iko tayari kuwapokea raia wengine wa Afghanistan wanaohitaji matibabu ya dharura na kuongeza kuwa hospitali zingine za Iran nazo pia ziko tayari kutoa huduma.

Hospitali ya Baqiyatullah

Kundu la kigaidi la ISISI au Daesh lilitangaza kuhusika katika hujuma za kigaidi dhidi ya misikiti ya Waislamu wa madhehebu ya Shia huko Kunduz na kisha Kandahar wakati wa Sala ya Ijumaa kwa muda wa wiki mbili mfululizo. Serikali ya Taliban imesema itachukua hatua dhidi ya magaidi hao wa ISIS ambao wameua na kujeruhi mamia ya Waislamu katika misikiti hiyo miwili.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imelaani hujuma hizo dhidi ya misikiti wakati wa Sala ya Ijumaa na kusema hiyo ni njama ya kuibua mifarakano baina ya Waislamu wa madhehebu ya Shia na Sunni.