Oct 22, 2021 09:54 UTC
  • Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Uturuki waelezea wasiwasi kuhusu kuongezeka ugaidi wa Daesh Afghanistan

Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Uturuki wamebainisha wasiwasi wao kuhusu kuongezeka vitendo vya ugaidi wa Daesh dhidi ya waumini katika misikiti ya Afghanistan ambavyo hadi sasa vimepelekea kuuawa makumi ya waumini waliokuwa wakitekeleza ibada ya swala ya Ijumaa katika misikiti hiyo.

Akizungumza kwa njia ya simu hapo jana Alkhamisi na waziri mwenzake wa mambo ya nje wa Uturuki, Hussein Amir Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema nchi za Kiislamu zinatakiwa kuwajibika zaidi katika kubabiliana na matukio ya ugaidi na hasa yale yanayotekelezwa na Daesh dhidi ya Waislamu.

Mapema mwezi huu Daesh ilitekeleza mashambulio tofauti ya kigaidi katika misikiti miwili ya Mashia wa Afghanistan katika miji ya Kandahar na Kunduz na kupelekea makumi ya waumini kuuawa katika mashambulio hayo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imelaani vikali mashambulio hayo na kusema yanalenga kupanda mbegu ya chuki na uhasama kati ya madhehebu tofauti ya Kiislamu huko Afghanistan na hivyo kuweka wazi jukumu kubwa ililonalo kundi la Taliban katika kulinda usalama wa raia na makundi tofauti ya kimadhedhebu ya nchi hiyo.

Ugaidi wa Daesh ndani ya msikiti Afghanistan

Amir Abdollahian pia ameashiria mkutano ujao wa nchi jirani na Afghanistan hapa mjini Tehran na kusema kikao hicho kitakuwa fursa nzuri kwa ajili ya nchi shiriki kubadilishana mawazo na fikra kuhusu namna ya kurejesha amani na utulivu wa kudumu katika nchi hiyo.

Kwa uapande wake Mevlut Cavusoglu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uturuki amebainisha wasiwasi wake kutokana na kuongezeka vitendo vya ugaidi huko Afghanistan na kusisitiza umuhimu wa kuchukuliwa hatua za dharura ili kuzuia kuongezeka ugaidi katika nchi hiyo.