Oct 24, 2021 04:33 UTC
  • Amir-Abdollahian: Mazungumzo ya nyuklia na kundi la 4+1 yataanza tena hivi karibuni

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, mazungumzo ya nyuklia na kundi la 4+1 yanatarajiwa kuanza tena hivi karibuni.

Hussein-Amir Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema hayo katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Khusrav Noziri, Katibu Mkuu  wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya ECO ambapo amesisitiza kuwa, karibuni hivi mazungumzo hayo ya nyuklia yataanza tena.

Katika mazungumzo hayo mbali na kuzungumzia suala la mazungumzo ya nyuklia ya Iran na Ulaya ameashiria pia uhusiano wa Iran na jumuiya hiyo na ulazima wa kutekelezwa baadhi ya mipango ya kimsingi na ya muda mrefu katika uga wa usafiri na uchukuzi, biashara na masuala ya kifedha.

Kuhusiana na matukio ya Afghanistan, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kusikitishwa kwake na matukio hayo ya kigaidi na kutoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya ECO hasa kwa kutilia maanani kwamba, Afghanistan ni mmoja wa wanachama muhimu wa jumuiya hiyo.

Kwa upande wake, Khusrav Noziri, Katibu Mkuu  wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi ya ECO sambamba na kutilia mkazo nafasi na mchango muhimu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika jumuiya hiyo ametoa wito wa kuendelezwa himaya na uungaji mkono wa Tehran kwa jumuiya hiyo muhimu katika eneo hili.