Oct 24, 2021 08:15 UTC
  • Spika wa Bunge la Iran awapongeza maspika wa nchi za Kiislamu kwa mnasaba wa Maulidi ya Mtume (saw)

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amewatumia ujumbe maspika wenzake katika nchi za Kiislamu akiwapa mkono wa kheri na baraka kwa mnasaba wa maadhimisho na sherehe za Maulidi ya Mtume Muhammad (saw).

Muhammad Baqir Qalibaf amesema katika ujumbe huo kwamba, anawatakia kheri, baraka na fanaka Waislamu kwa mnasaba wa maadhimisho ya Maulidi na kumbukumbu ya tukio la kuzaliwa Mtume Muhammad (saw). Amesema inatarajiwa kuwa chini ya kivuli cha mafundisho ya Uislamu, Qur'ani tukufu na Suna za Mtume (saw) kutashuhudiwa juhudi za kuimarisha mshikamano na udugu katika Umma wa Kiislamu. 

Mapema, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Sayyid Ebrahim Raisi alikuwa tayari ametuma salamu maalumu na mkono wa baraka na fanaka kwa viongozi wa nchi za Kiislamu kwa mnasaba wa maadhimisho ya Maulidi na siku ya kuzaliwa Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad (saw) na Wiki ya Umoja wa Kiislamu. 

Katika jumbe hizo Sayyid Ebrahim Raisi amesema: Ni matarajio kwamba katika siku hizi adhimu na zenye baraka tele za Maulidi na sherehe ya kuzaliwa ruwaza njema, Muhammad (saw) tutafanya jitihada kubwa za kuimarisha mahusiano endelevu na imara kwa ajili ya kunyanyua juu zaidi Uislamu na kueneza sira na mienendo ya Mtume wa Rehma, Muhammad (saw) kwa kutumia mafundisho ya dini hiyo yanayotukutanisha sisi sote pamoja na azma yetu ya udugu wa kiimani.

Ni vyema kukumbusha hapa pia kwamba makumi ya wasomi na wanafikra wa Kiislamu kutoka nchi mbalimbali ambao wanashiriki katika Mkutano wa Kimataifa ya Umoja wa Kiislamu wamekutana na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei hapa mjini Tehran muda mfupi uliopita katika majlisi ya Maulidi ya Mtume (saw). Habari kuhusu mkutano huo itakujieni katika matangazo yetu yajayo. 

Leo tarehe 17 Mfunguo Sita Rabiu Awwal 1443 Hijria kwa mujibu wa nukuu za maulama na wanahistoria wengi wa Kiislamu, inasadifiana na siku aliyozaliwa Mtume wa Mwisho wa Mwenyezi Mungu, Muhammad bin Abdullah (saw) na mjukuu wake mwema, Imam Ja'far al Swadiq (as).

Mtume Muhammad (saw) alizaliwa tarehe 17 Mfunguo Sita Mwaka wa Tembo katika mji mtakatifu wa Makka. 

Tags