Oct 24, 2021 10:27 UTC
  • Iran na Uturuki; ulazima wa kufanyika juhudi za kuboresha uhusiano wa kiuchumi

Katika siku za hivi karibuni maafisa na viongozi wa Jamhuri ya Kiislamuu ya Iran na Uturuki wamekuwa na mazungumzo ya pande mbili ya ana kwa ana na kwa njia ya simu ambapo wamekuwa wakisisitizia udharura wa umuhimu wa uhusiano wa nchi mbili katika nyanja za kiuchumi na ushirikiano wa kieneo kwa shabaha ya kuleta amani na uthabiti, na wakati huo huo kuzuia hatua zozote zile zenye lengo la kuleta mizozo na mivutano.

Hussein Amir-Abdollahiyan, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisisitiza katika mazungumzo yake kwa njia ya simu na Mevlut Cavusoglu, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uturuki juu ya sera za kigeni za Tehran ambazo zimejengeka juu ya msingi wa kuheshimiwa mamlaka ya kujitawala na ardhi yote ya mataifa jirani na kutoruhusu chokochoko na uafiriti wa wale wasiolitakia mema suala la uhusiano mzuri na ujirani mwema.

Kabla ya hapo, Ahmad Vahidi, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Iran alikutana na kufanya mazungumzo hapa mjini Tehran na  Suleyman Soylu, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki ambapo aliutaja uhusiano wa nchi mbili hizi kuwa ni mzuri mno na kubainisha kwamba, Iran na Uturuki zinataka kustawishwa zaidi uhusiano na ushirikiano wao katika nyuga zote. Kwa upande wake Suleyman Soylu, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki alisema, uhusiano wetu na Iran siyo wa kidiplomasia tu, bali ni wa kirafiki na kidugu. Aidha alieleza matumaini aliyonayo ya kufunguliwa ukurasa mpya katika uhusiano huu ambao utakuwa ni kwa maslahi ya Tehran na Ankara na kukwamisha njama zote za maadui.

Hussein Amir-Abdollahiyan, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Mevlut Cavusoglu, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Uturuki

 

Uturuki ni mmoja wa majirani muhimu zaidi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Mataifa haya mawili yana maslahi ya mengi ya pamoja ya kisiasa na kiusalama na katika kipindi cha zaidi ya miaka 400 yamekuwa yakitilia mkazo suala la ujirani mwema.

Mtazamo jumla kwa historia ya uhusiano wa Iran na Uturuki unaonyesha kuwa, uchumi, uhusiano wa kibiashara na nishati ni miongoni mwa mihimili ya ushirikiano; na mkabala na hilo, masuala ya kisiasa na jiopolitiki ni miongoni mwa sababu za hitilafu baina ya nchi mbili hizii. Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana uhusiano wa Iran na Uturuki katika vipindi tofauti ulikumbwa na hali ya muachano kutokana na sababu za ushindani na vilevile kuathirika na matukio ya kieneo na kimataifa.

Pamoja na hayo ushindani na hitilafuu hizi hakuna wakati ambao zilipelekea au kuwa sababu ya kuzorota uhusiano wa nchi mbili na hivyo kusimamisha ushirikiano wao. Viongozi wa Iran na Uturuki daima  wamekuwa wakisisitizia ulazima wa kuendelezwa mazungumzo na ushirikiano baina ya pande mbili. Kwa mfano, Uturuki ni miongoni mwa mataifa ambayo yalitetea haki ya Iran ya kunufaika na teknolojia ya kisasa ya nishati ya nyuklia kwa malengo ya amani. Iran nayo, katika mapinduzi ya 2016 nchini Uturuki ilisimama upande wa serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan.

Kwa muktadha huo, maslahi ya pande mbili katika kupanua ushirikiano yapo katika nyanja zote na filihali nchi hizi zimekuwa na ushirikiano wa karibun mno kuhusiana na masuala kama ya usalama wa mipakani, vita dhidi ya magendo ya madawa ya kulevya na ya binadamu, na vile vile vita dhidi ya ugaidi.

Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika moja ya mazungumzo yake na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki

 

Hata  hivyo, uhusiano wa kiuchumi baina ya Iran na Uturuki katika miaka ya hivi karibuni umedorora kutokana na sababu zilizo nje uwezo wa mataifa haya kama vile vikwazo vya upande mmoja na vya kidhalimu vya Marekani dhidi ya Iran na janga la virusi vya Corona. Mwenendo huu hauna maslahi kabisa kwa mataifa yote mawili. Iran na Uturuki zilitabiri kuongeza zaidi mabadilishano ya kibiashara kati yao hadi kufikia dola bilioni 340 mwaka 2015, hata hivyo mabadilishano ya kibiasdhara ya kiwango cha juu kabisa baina ya nchi hizi yanarejea katika mwaka 2012 ambapo kilifikia dola bilioni 21. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kiwango hicho kimepungua kwa dola bilioni 10.

Muhammad Farazmand, balozi wa Jamhhuri ya Kiislamu ya Iran huko Ankara Uturuki sanjari na kuashiria kwamba, Tehran na Ankara zinaweza kudhamini mahitaji ya kila mmoja anasema: Nchi mbili hizi ambazo zinakabiliwa na vitisho na vikwazo vya madola makubwa, zina uwezo mkubwa wa kutosha wa kiuchumi na hivyo zinaweza kufanya biashara baina yao kwa kuanzisha mikakati ya pande mbili pasi na kuhitajia fedha za kigeni.

Hapana shaka kuwa, katika mazingira ya hivi sasa na umuhimu unaoongezeka kila uchao wa mchango wa uchumi katika siasa ambapo ni moja ya sababu za mataifa hayo kuwa na mitazamo mimoja hasa kwa kutilia maanani kwamba, mataifa haya ni jirani, hatua yoyote ile ya kuchelewa kuboresha na kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara baina ya pande mbili itakuwa ni kwa madhara kwa serikali hizi mbili na kwa wanaharakati wa sekta ya uchumi wa nchi mbili hizi.

Ukweli wa mambo ni kuwa, nafasi ya jiopolitiki ya Iran na Uturuki ni sababu muhimu zaidi ya kushirikiana kiuchumi na kibiashara pande mbili, na mabadilishano ya kibiashara na kiuchumi yenye mgawo wa pata nipate na  wa nusu kwa nusu sambamba na kupanuliwa ushirikiano katika sekta ya viwanda, kilimo, utoaji huduma, utalii, mafuta, gesi, petrokemikali na vilevile kutumiwa fursa za uwekezaji katika mataifa mawili, ni mambo ambayo yanaweza kuzingatiwa na kupewa umuhimu katika fremu hii.