Oct 24, 2021 15:17 UTC
  • Kiongozi Muadhamu: Mazazi ya Mtume (SAW) yalifungua ukurasa mpya wa maisha ya mwanadamu

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesema kuzaliwa Mtume mtukufu Muhammad (SAW) kulifungua ukurasa mpya katika maisha ya mwanadamu.

Ayatullah Ali Khamenei amesema hayo leo Jumapili katika mkutano wake na viongozi wa mihimili mitatu ya serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na washiriki wa mkutano wa 35 wa Wiki ya Umoja wa Kiislamu hapa jijini Tehran.

Katika hotuba yake aliyotoa mbele ya hadhira hiyo kwa mnasaba wa maadhimisho ya Maulidi ya kukumbuka kuzaliwa Mtume Muhammad (SAW) na vile vile kumbukizi ya mazazi ya Imam wa Sita wa Waislamu wa Kishia, Ja'afar Sadiq (AS), Kiongozi Mudhamu amesema umoja wa Waislamu ni wajibu uliobainishwa wazi kwenye Qurani tukufu, na wala si suala la kimkakati. 

Kiongozi Muadhamu akihutubu

Amebainisha kuwa, Waislamu hawapaswi kuungana na kusimama pamoja wakati wa matukio fulani maalumu pekee, bali wanapaswa kushirikiana nyakati zote na kustawi pamoja, kwani hilo ni jambo la dharura.

Ayatullah Khamenei ameeleza kuwa:  Mazazi ya Mtume (SAW) yamefungua ukurasa mpya wenye kuchanua katika maisha ya mwanadamu, kuashiria kuanza kwa enzi mpya yenye utakasifu wa kiroho na vile vile Rehema kwa jamii ya mwanadamu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, kadhia ya Palestina ndilo suala kuu la kuwaunganisha Waislamu, na kwamba iwapo umoja huo utapatikana, suala la Palestina litapatiwa ufumbuzi kwa njia mwafaka na bora zaidi.

Amefafanua kwa kusema: Kadri tunavyolichukuliwa kwa uzito na mazingatio suala la haki za Wapalestina, ndivyo tunavyozidi kukurubiana na kuungana kama umma wa Kiislamu.

Amesema, kwa masikitiko baadhi watawala wa nchi fulani za Kiarabu wamefanya kosa na dhambi kwa kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni na kidhalimu wa Israel, hatua ambayo inahujumu umoja wa Waislamu.

Maafisa wa serikali ya Iran na wageni walioshiriki Wiki ya Umoja wakifuatilia hotuba ya Kiongozi Muadhamu

Kiongozi Muadhamu ameongeza kuwa, "Suala la kuwagawa Waislamu katika misingi ya madhehebu limepenya kwenye siasa za Marekani kwa miaka kadhaa sasa. Ingawaje maadui wamesimama dhidi ya Uislamu wenyewe, lakini hawaachani kabisa na masuala ya Masunni na Mashia."

Ameashiria wimbi la mashambulio ya kigaidi ya hivi karibuni dhidi ya misikiti nchini Afghanistan na kueleza kuwa, hujuma hizo za umwagaji damu ni mfano wa namna vikaragosi vya Marekani vinajaribu kuibua mifarakano popote pale katika ulimwengu wa Kiislamu.   

 

Tags