Oct 25, 2021 02:34 UTC
  • Shamkhani: Israel itenge bajeti ya kutosha ya kukarabati hasara za majibu ya Iran

Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel uanze kufikiria kutenga bajeti ya hasara kubwa zitakazosababishwa na majibu makali ya Iran.

Ali Shamkhani amesema hayo kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, ikiwa ni kujibu upayukaji mpya wa utawala wa Kizayuni ambao umedai kuwa, Israel imetenga fedha maalumu za kufanya operesheni za kiuadui dhidi ya Iran.

Shamkhani amesema katika ujumbe wake huo kwamba, badala ya utawala wa Kizayuni kufikiria kutenga dola bilioni 1.5 za kufanya uharibifu dhidi ya Iran, unapaswa ufikiria kwanza kutenga makumi ya maelfu ya dola za kukarabati hasara kubwa itakayopata Israel kutokana na majibu makali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ali Shamkhani

 

Ikumbukwe kuwa, siku chache zilizopita, Kikosi cha Anga cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kilifanya mazoezi makubwa yaliyopewa jina la 'Duru ya 10 Uwezo wa Anga wa Waliojitolea Kulinda Anga ya Wilayat'. Mazoezi hayo yalizinduliwa rasmi kwa kutamkwa ' Ya Muhammad Ya Rasulallah SAW.

Taarifa zilisema kuwa, mazoezi hayo ambayo yameanza siku ya Alkhamisi, yameshirikisha vituo vya ndege za kijeshi katika maeneo mbali mbali ya Iran. Akizungumza na waandishi habari, Naibu Kamanda wa Kikosi cha Jeshi la Anga la Iran Mehdi Hadian alisema kuwa, mazoezi hayo yamefanyika katika eneo kubwa la Iran. Aliongeza kuwa, moja ya malengo ya luteka hiyo ni kuonesha uwezo mkubwa wa kivita wa kikosi hicho katika mazingira halisi ya kivita. 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza mara kwa mara kuwa uwezo wake mkubwa wa kijeshi si tishio kwa nchi yoyote na kwamba sera zake za ulinzi ni kwa ajili ya kukabiliana na maadui tu.

Tags