Oct 25, 2021 10:30 UTC
  • Sisitizo la Kiongozi Muadhamu kuhusu udharura wa kubainishwa umuhimu wa umoja katika Ulimwengu wa Kiislamu

Akizungumza Jumapili kwa mnasaba wa kuzaliwa Mtume (saw) na mjukuu wake Imam Jaffar as-Swadiq (as) mbele ya hadhara ya viongozi wa ngazi za juu wa mfumo wa Kiislamu na wageni walioshiriki katika kikao cha kimataifa cha Wiki ya Umoja wa Kiislamu hapa mjini Tehran, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema umoja wa Kiislamu ni msingi na faradhi ya Kiislamu na kwamba lengo kuu la utamaduni mpya wa Kiislamu haliwezi kufikiwa bila kuwepo umoja wa Shia na Suni.

Amesema kupatikana haki ya jamii ya Kiislamu na umoja wa Waislamu ni majukumu mawili muhimu yanayopaswa kutekelezwa na Umma wa Kiislamu katika ulimwengu wa leo. Kwa hakika umoja ni ngome na kiegemezi muhimu sana kilicho na manufaa mengi kwa Umma wa Kiislamu, lakini kama alivyosema Kiongozi Muadhamu, leo nchi nyingi za Kiislamu zimeghafilika na suala hilo muhimu. Hii ni katika hali ambayo umoja ni miongoni mwa nguzo muhimu zaidi za nguvu ya Ulimwengu wa Kiislamu inayodhamini mahitaji na kutatua matatizo yanayowakabili Waislamu, zikiwemo njama za maadui.

Kwa mtazamo huo umoja wa Kiislamu unakusudia kufikia malengo mawili makuu.

Lengo la kwanza ni kulinda thamani na utambulisho wa Kiislamu na kunyanyua nafasi ya nchi za Kiislamu kitaifa, kieneo na kimataifa.

Lengo la pili ni kueneza fikra na mafundisho aali na ya ukombozi ya Kiislamu ambayo yanaimarisha mirengo ya mapambano ya Kiislamu katika kukabiliana na njama za maadui wa Uislamu na kuzuia ubeberu wa madola ya kikoloni duniani.

Baadhi ya wageni walioshiriki kikao cha Wiki ya Umoja wa Kiislamu mjini Tehran

Kwa masikitiko makubwa historia ya Kiislamu imejaa matukio yanayothibitisha ukweli mchungu kwamba kumekuwepo makundi potovu ya kidini na kisiasa ambayo yamekuwa yakifuatilia kudhoofisha umoja wa Kiislamu na kuibua mifarakano katika Umma wa Kiislamu. Leo hii pia tunashuhudia harakati haribifu za makundi hayo katika sura mpya ambapo viongozi wa baadhi ya nchi za Kiislamu wanapeana mikono ya urafiki kwa maadui badala ya kuimarisha umoja na mshikamano kati ya Waislamu.

Kuhusu suala hilo, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amekemea kitendo cha baadhi ya nchi za Kiislamu katika eneo la Asia Magharibi kufuatilia siasa za kuwa na uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel ambao unaendelea kukandamiza wananchi wa Palestina wasio na hatia na kukanyaga wazi wazi thamani na matukufu yao ya Kiislamu. Kiongozi Muadhamu amaesema hiyo ni dhambi na kosa kubwa na kuongeza: Serikali hizi zinapasa kuachana na harakati na njia hiyo iliyo dhidi ya umoja wa Kiislamu, na kufidia makosa yao makubwa katika uwanja huo.

Hali ya hivi sasa ya Ulimwengu wa Kiislamu inaonyesha wazi ni kwa kiasi gani kutokuwepo umoja miongoni mwa Waislamu kunaweza kudhuru maslahi yao na kuwasababishia matatizo yasiyomalizika. Hii ni katika hali ambayo tiba ya matatizo hayo inapatikana kirahisi katika umoja na udugu wa Waislamu.

Katika kubainisha nukta hiyo muhimu, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria njama na juhudi zinazofanywa na Marekani na vibaraka wake katika eneo kwa ajili ya kueneza fitina katika kila pembe ya Ulimwengu wa Kiislamu na kusema lengo kuu la maadui ni kutaka kupanua zaidi pengo la mifarakano na migawanyoko iliyopo kati ya Waislamu. Amesema suala hilo ndilo limempelekea aendelee kusisitiza juu ya udharura wa kuwepo umoja na mshikamano kati ya Waislamu na kuongeza: Leo hii Wamarekani wanazungumzia suala la Shia na Suni katika hali ambayo wao wanapinga asili ya Uislamu.

Ameendelea kusema: Milipuko ya kusikitisha na inayomfanya mtu alie kwa uchungu iliyotokea katika siku za karibuni katika misikiti ya Afghanistan na dhidi ya Waislamu waliokuwa wakifanya ibada katika misikiti hiyo ni miongoni mwa matukio hayo ambayo yamesababishwa na Daesh, na awali Wamarekani wenyewe tayari walikuwa wamekiri wazi wazi kuwa wao ndio walioanzisha Daesh.

Baadhi ya jinai za Daesh katika misikiti ya Afghanistan

Tukio jingine chungu na kubwa ambalo limekuwa likiendelea katika ulimwengu wa Kiislamu kwa zaidi ya nusu karne sasa na ambalo linatokana na kutokuwepo umoja katika Umma wa Kiislamu, ni kuendelea kukaliwa kwa mabavu ardhi za Wapalestina na utawala ghasibu wa Israel. Hayo ni licha ya kwamba suala hilo lina umuhimu mkubwa wa kisiasa katika ulimwengu wa Kiislamu bila kujali madhehebu, rangi na makabila ya Waislamu. Suala hilo lina umuhimu mkubwa kadiri kwamba Kiongozi Muadhamu amesisitiza kuwa hicho ndicho kipimo kikuu cha kuimarisha umoja wa Waislamu na kusema kadiri juhudi zinavyofanyika kwa ajili ya kupigania haki za Wapalestina ndivyo umoja na mshikamano unavyozidi kuimarika miongoni mwa Waislamu. Jambo lenye lenye umuhimu hapa ni kuwa hitajio muhimu zaidi la Umma wa Kiislamu katika ulimwengu wa leo na katika mazingira tata ya hivi sasa ni kunyanyuliwa kiwango cha mwamko wa kisiasa wa Waislamu kuhusu umuhimu wa kuwepo umoja katika ulimwengu wa Kislamu.

Hotuba ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu suala hilo ni yenye umuhimu mkubwa katika kuleta mwamko kati ya Waislamu na wakati huo huo inakumbushia nukta hii kwamba wanafikra na wasomi wa Kiislamu wana jukumu zito katika uwanja huo.