Oct 26, 2021 12:27 UTC
  • Iran: Tunaendelea kufanya mashauriano ya kiusalama na serikali mpya ya Afghanistan

Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran inaendelea kufanya mashauriano na serikali mpya ya Afghanistan hasa katika masuala ya kuleta amani, utulivu na usalama wa kudunu nchini humo.

Hossein Amir-Abdollahian amesema hayo leo Jumanne baada ya kuonana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Mahmoud Gureishi na kuongeza kuwa, kuundwa serikali ya pande zote itakayoshirikisha makundi yote ndiyo njia bora ya utatuzi wa matatizo ya Afghanistan.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran vile vile amesema kuwa, tumekubaliana na nchi ndugu na rafiki ya Pakistan  kuwa na msimamo mmoja katika kikao cha mawaziri wa mambo ya nje wa nchi jirani na Afghanistan kinachotarajiwa kufanyika kesho Jumatano hapa Tehran.

Wakati huo huo mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa yametangaza kuwa, zaidi ya nusu ya wananchi wa Afghanistan wanakabiliwa na hali mbaya ya ukosefu wa chakula.

Taarifa ya mashirika hayo ya Umoja wa Mataifa iliyotolewa leo imeeleza kuwa, zaidi ya wananchi milioni 22 wa Afghanistan watakabiliwa na hali mbaya ya ukosefu wa chakula katika msimu wa baridi mwaka huu.

Viongozi wa Taliban, Afghanistan

 

Sehemu nyingine ya taarifa hiyo imeeleza kuwa, kwa sasa Afghanistan ni moja ya nchi zinazokabiliwa na tatizo kubwa la mgogoro wa kibinadamu.

Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) limesema kuwa, katika msimu huu wa baridi ulioko mbeleni, mamilioni ya Waafghanistan watalazimika kuchagua baina ya kuhajiri au kufa kwa njaa.

Omar Abdi Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF) alisema hivi karibuni kuwa, mfumo wa afya na huduma za kijamii nchini Afghanistan unakaribia kusambaratika.

Tags