Oct 27, 2021 08:12 UTC
  • Mkutano wa pili wa Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa mataifa jirani na Afghanistan+Russia waanza Tehran

Mkutano wa pili wa Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa mataifa jirani na Afghanistan+Russia umeanza kufanyika hapa mjini Tehran kwa shabaha ya kujadili changamoto mbambali zinazoikabili nchi hiyo baada ya majeshi ya Marekani kuondoka nchini humo na wanamgambo wa Taliban kuchukua hatamu za uongozi wa nchi.

Hussein Amir-Abdollahiyan, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, mkutano huu unahudhuriwa na Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa mataifa 6 jirani na Afghanistan+Russia ukihudhuriwa na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Iran Muhammad Mokhber.

Amir-Abdollahiyan amebainisha kuwa, lengo la mkutano huu unaofanyika katika makao makuu ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ni kujikita zaidi katika kujadili hali na mazingira mapya inayokabiliwa nayo hivi sasa nchi ya Afghanistan.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameongeza kuwa, ana matarajio kwamba, kwa kuweko sauti moja mataifa haya yanaweza kuifikishia ujumbe jamii ya kimataifa kile kinachojiri nchini humo.

Image Caption

 

Katika upande mwingine, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa, Marekani inapaswa kubeba dhima na majukumu mkabala na maafa ya Afghanistan.

Mkutano wa kwanza kuhusu Afghanistan ulifanyika kwa njia ya intaneti kwa uongozi wa Pakistan Julai mwaka huu na uliwaleta pamoja wadau wa Afghanistan na kimataifa pamoja na wahusika wengine wa mchakato wa kutafuta amani Afghanistan.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Wakati huo huo mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa yametangaza kuwa, zaidi ya nusu ya wananchi wa Afghanistan wanakabiliwa na hali mbaya ya ukosefu wa chakula.

Tags