Nov 09, 2021 02:23 UTC

Luteka ya pamoja ya Dhulfiqar 1400 ya Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilianza siku ya Jumapili kwa jina takatifu la 'Ya Rasulullah (saw).'

Luteka hiyo inayovishirikisha vikosi mbalimbali vya anga, nchi kavu na majini vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatekelezwa katika pwani ya Makran kusini mwa Iran.

Akifafanua ujumbe wa luteka hiyo kwa watu wa Iran na pia nchi rafiki na vilevile maadui wa Iran, Brigedia Jenerali Taqikhani, Msemaji wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: Jeshi na vikosi vyake vyote vinapasa kuwa tayari siku zote ambapo kulinda utayari huo katika viwango vyote ndiko kunadhamini amani ya kudumu nchini na katika mipaka yote ya Jamhuri ya Kiislamju ya Iran.

Ukubwa wa eneo la luteka, usimamiaji wa kiwango cha juu wa habari za kijeshi, matumizi ya zana za kisasa zilizotengenezwa ndani ya nchi, kutumika ndege zizizo na rubani, zana za kijeshi za kielektroniki na mifumo ya kamandi ya udhibiti wa jeshi ni miongoni mwa masuala muhimu na maalumu yanayoonekana katika luteka hiyo.

Luteka ya Dhulfiqar

Nukta ya kwanza muhimu ya luteka hiyo ni kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwa nchi yenye nguvu kubwa ya kijeshi Asia Magharibi (Mashariki ya Kati) ina malengo ya kistratijia kwa ajili ya kulinda usalama wa mipaka yake na kwa hivyo daima inapasa kuwa tayari kwa ajili ya kukabiliana na tishio lolote lile.

Akisisitiza juu ya nukta hiyo muhimu, msemaji wa luteka hiyo amesema: Tunawaonya maadui wasije wakawa na fikra yoyote ya kipumbavu kuhusu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mipaka yake.

Nukta ya pili muhimu katika uwanja huo ni kufanyika luteka ya Dhulfiqar 1400 katika pwani ya Makran jambo ambalo lina umuhimu mkubwa katika kulinda usalama wa eneo.

Jamhuri ya Kiislamu daima imekuwa ikitangaza kuwa kulindwa usalama wa Bahari ya Oman, Lango Bahari la Hormuz na Ghuba ya Uajemi, zikiwa njia kuu muhimu za majini kimataifa, kuna umuhimu mkubwa. Mtazamo wa Iran katika uwanja huo ni kulindwa usalama huo na nchi za eneo bila kuingiliwa na nchi za kigeni. Hii ni kutokana na ukweli kuwa uwepo wa nchi za kigeni katika eneo na hasa Marekani badala ya kudhamini usalama, uwepo huo wenyewe ndio chanzo cha kuvurugwa usalama wa eneo.

Nukta ya tatu inayobainisha umuhimu wa luteka ya Dhulfiqar 1400 ni kutumika katika luteka hiyo zana nzito na za kisasa kabisa zikiwemo droni na mifumo ya anga ambazo zote zimetengenezwa humu humu nchini na wataalamu wa Kiirani.

Luteka ya Dhulfiqar

 

Kutekelezwa operesheni za usiku na katika mazingira ya kiza kikubwa ni sehemu nyingine muhimu ya luteka ya Dhulfiqar 1400.

Taasisi ya utafiti wa kiulinzi na kiusalama ya Uingereza imetoa ripoti ikitangaza kuwa maendeleo makubwa yaliyopatikana katika sekta ya ulinzi ya Iran ni mapinduzi makubwa ya kiufundi.

Jack Watling, mtafiti katika taasisi ya huduma za kifalme nchini Uingereza anasema: Iran inaweza kuwa moja ya nchi zilizo na uwezo mkubwa wa kijeshi wa kuiwezesha kukabiliana na tishio lolote la kijeshi. Kwa msingi huo maadui wa Iran wanapasa kufanya mahesabu mazuri kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kijeshi dhidi yake.

Taasisi ya kifikra ya Enterprise ya nchini Marekani karibuni pia iliandika kuhusiana na nguvu ya kijeshi ya Iran na kusema: Mfumo wa kiulinzi wa Iran umesimama juu ya msingi wa uzoefu wa kijeshi kwa lengo la kutafuta ufumbuzi wa kukabiliana na changamoto za kijeshi katika eneo.

Sehemu ya Luteka ya Dhulfiqar

Kwa muhtasari ni kuwa kufanyika luteka hiyo kubwa ya jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kunadhihirisha uwezo wake mkubwa wa kijeshi katika kubaliana na vitisho vya maadui. Ni kwa kuzingatia nukta hiyo muhimu ndipo ujumbe wa luteka ya Dhulfiqar 1400 ukatangazwa kuwa ni onyo kwa maadui na sisitizo la usalama kwa wote katika eneo.