Nov 16, 2021 11:43 UTC
  • Iran: Tuko tayari kushirikiana na nchi za magharibi mwa Afrika kupambana na ugaidi

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu y Iran ameelezea kusikitishwa kwake na kupoteza maisha na kujeruhiuwa idadi kubwa ya raia wa Burkina Faso katika shambulio la hivi karibuni la kigaidi na kusisitiza kuwa, Tehran iko tayari kushirikiana na nchi za magharibi mwa Afrika katika vita dhidi ya ugaidi.

Kwa mujibu wa taarifa ya leo Jumanne ya Idara ya Upashaji Habari ya Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Saeed Khatibzadeh ameelezea kusikitishwa sana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mashambuliio ya kigaidi huko Burkina Faso na kusema kuwa, Tehran iko tayari kushirikiana na Burkina Faso na nchi za magharibi mwa Afrika kupambana na vitendo vya kikatili vya magaidi.

Msemaji huyo wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran aidha ametoa mkono wa pole kwa serikakli na wananchi wa Burkina Faso hasa watu wa familia za wahanga wa shambulio hilo la kigaidi na kusema, ana matumaini hatua kali zitachukuliwa dhidi ya magaidi waliofanya jinai hiyo.

Vitendo vya kigaidi vimesababisha maafa makubwa magharibi mwa Afrika ikiwemo Burkina Faso

 

 

Jana Jumatatu kuliripotiwa habari ya kuuawa watu 20 wakiwemo askari wasiopungua 19 wa serikali ya Burkina Faso katika shambulio la kigaidi la kaskazini mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Maxim Kone, Waziri Usalama wa Burkina Faso alithibitisha habari hizo na kuongeza kuwa, wanajeshi 19 wa Burkina Faso wameuwa katika shambulizi hilo la Jumapili, baada ya magaidi kuvamia kambi ya jeshi ya Inata katika mkoa wa Soum, kwenye eneo la Sahel.

Alisema operesheni ya kukabiliana na magaidi hao ingali inaendelea, na kuwataka wakazi wa maeneo hayo kuwa macho na kushirikiana kwa karibu na maafisa usalama kuwatambua waliohusika na jinai hiyo.

Tags