Nov 19, 2021 07:52 UTC

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu si kitu kingine ghairi ya muendelezo wa sera zilizogonga ukuta za Donald Trump.

Saeed Khatibzadeh alisema hayo jana Alkhamisi na kueleza bayana kuwa, "Iran inavitazama vikwazo hivyo vya Marekani dhidi ya Iran kama jitihada za kuendeleza sera iliyofeli ya mashinikizo ya kiwango cha juu zaidi ya (aliyekuwa rais wa Marekani, Donald) Trump."

Khatibazadeh sambamba na kusisitiza kuwa vikwazo hivyo ni haramu na vinavyokiuka sheria, amebainisha kuwa, Washington inachukua hatua za namna hii kutokana na kukata kwake tamaa.

Kauli ya Khatibazadeh ni radiamali kwa hatua ya Wizara ya Hazina ya Marekani kuwaweka Wairani sita na taasisi moja ya Kiirani katika orodha ya mpya ya vikwazo, kwa kisingizio kuwa walijaribu kuingilia uchaguzi wa Marekani wa mwaka jana, 2020.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ameeleza kuwa, Marekani inaendelea kutumia vikwazo kuzikomoa nchi nyingine duniani katika hali ambayo, yenyewe ina rekodi ndefu ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi zingine duniani.

Wakati huo huo, Saeed Khatibzadeh amelaani vikali matamshi ya uingiliaji wa mambo ya ndani ya nchi nyingine yaliyotolewa hivi karibuni na Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Ufaransa, Anne-Claire Legendre, aliyeutaka Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) eti uipe Iran 'ujumbe wa nguvu' na kuitaka Tehran eti irejee katika utekelezaji wa majukumu yake yanayofungamana na makubaliano ya nyuklia ya JCPOA bila kupoteza muda.

Tags