Nov 19, 2021 15:20 UTC
  • Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran: Sahihi ya rais wa Marekani si ya kutegemewa

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema, sharti la kukubaliwa Marekani kurudi kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ni kuondoa Washington kwa namna athirifu, itakayoweza kuthibitika na kwa wakati mmoja vikwazo vyote ilivyoiwekea Iran na kwamba sahihi ya rais wa Marekani haiwezi kutegemewa.

Saeed Khatibzadeh ameyasema hayo leo katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran IRIB alipozungumzia masharti ya Iran kuhusiana na kurejeshwa Marekani katika JCPOA na akaongezea kwa kusema, "kuondoa vikwazo kwa namna athirifu, itakayoweza kuthibitika na kwa mpigo ndio masharti ya kurejea Marekani katika JCPOA na hili ndilo lengo letu katika mazungumzo ya Vienna."

Khatibzadeh ameendelea kueleza kwamba, ikiwa Marekani itaingia kwenye mazungumzo ya Vienna na muelekeo huo na itakuwa tayari kuviondoa vikwazo vyote kwa pamoja na ikawezekana kulithibitisha hilo, hakuna shaka yoyote mwafaka utaweza kufikiwa katika muda mfupi kabisa.

Hata hivyo msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametanabahisha kwa kusema: "Bila shaka tunataka kuwepo na hakikisho kwamba Marekani haitakuja kuzikejeli tena na kuzifanyia mzaha sheria za kimataifa."

Khatibzadeh amesisitiza kuwa, Marekani, ikiwemo serikali ya sasa, imeonyesha kuwa haina mwamana wa kutekeleza inayoyaahidi; na sahihi ya rais wa Marekani, licha ya wanavyodai wenyewe, haina thamani wala haiwezi kutegemewa; na kwa sababu hiyo, ni jambo la kutarajiwa kuona Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na timu yake ya mazungumzo zinatilia mkazo ulazima wa kupatiwa hakikisho.

Ikumbukwe kuwa, tarehe 8 Mei 2018, aliyekuwa rais wa Marekani Donald Trump alichukua hatua ya upande mmoja na ya ukiukaji sheria ya kuiondoa nchi yake katika makubaliano ya kimataifa ya nyuklia ya JCPOA na kurejesha tena vikwazo vya nyuklia ambavyo Washington ilikuwa imeiwekea Tehran.../

Tags