Nov 20, 2021 13:43 UTC
  • Vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya Iran kwa kisingizio cha kuingilia uchaguzi

Wizara ya Fedha ya Marekani juzi Alhamisi ilitangaza kuwa imeyaweka katika orodha yake ya vikwazo majina ya shakhsia sita na shirika moja la Iran kwa kisingizio cha kuingilia uchaguzi wa rais wa Marekani. Ofisi inayosimamia fedha ya taasisi hiyo ya Marekani imesema kuwa imeyaweka katika orodha yake ya vikwazo majina ya watu sita na taasisi moja ya Iran kwa kile ilichokitaja kuwa kujaribu kuathiri uchaguzi wa rais wa Marekani wa mwaka 2020.

Taarifa ya Wizara ya Fedha ya Marekani imedai kuwa, Marekani imebaini kujipenyeza na hujuma za kimtandao zilizofanywa na maajenti wanaofadhiliwa na nchi mbalimbali wakiwemo maajenti wa Iran. Imeongeza kuwa, maajenti hao walikuwa na lengo la kuzusha hililafu na kudhoofisha imani ya wapiga kura kwa mchakato wa uchaguzi nchini Marekani. "Watu hao walieneza taarifa za uwongo katika mitandao ya kijamii na kutuma barua pepe za vitisho na video bandia," imedai taarifa hiyo.   

Washington imeiwekea Iran vikwazo vipya kinyume na ahadi za huko nyuma za serikali ya Biden za kubadili hatua na mienendo ya Marekani mkabala na Iran; hata hivyo serikali ya Washington ingali inashikilia sera hizo zilzogonga mwamba za mashinikizo ya kiwango cha juu dhidi ya Iran. Kuhusiana na hilo, Jen Psaki Msemaji wa White House ameashiria baadhi ya ripoti kuhusu uwezekano serikali ya Biden kufanya jitihada za kufikia mapatano ya muda na Iran na kueleza kuwa, wenzo wa vikwazo wa Marekani dhidi ya Iran uko pale pale na haujabadilika.  

Jen Psaki, Msemaji wa White House 

Jambo jingine la kutilia maanani kuhusu kuwekewa vikwazo shakhsia hao sita na taasisi ya Iran ni kisingizo kinachotumiwa na Marekani katika uwanja huo yaani eti "waliingia uchaguzi wa rais wa Marekani". Marekani inafanya kila linalowezekana kuzituhumu nchi mahasimu wake kwamba ziliiingia uchaguzi mkuu wa nchi hiyo mwaka uliopita. Hii ni katika hali ambao, Marekani yenyewe ina rekodi ya muda mrefu katika kuingilia masuala ya ndani ya nchi mbalimbali duniani ukiwemo uingiliaji wake wa moja kwa moja na usio wa moja kwa moja katika chaguzi mbalimbali pamoja na kufanya njama za kuziondoa madarakani serikali hususan kufanya mapinduzi ya rangi na kadhalika. 

Mara hii pia serikali ya Biden kwa kuibua chochoko na tuhuma zisizo na msingi, inatafuta kisingizio cha kuzidisha mashinikizo dhidi ya Iran. Tuhuma kama hizo za Washington hazikuwa dhidi ya Iran pekee bali katika miaka ya karibuni Marekani imeziandama pia Russia na China kwa tuhuma kama hizo. Wakati huo huo tukitupia jicho historia ya Marekani tunaona kuwa, Washington imeingia kwa njia ya moja kwa moja na isiyo ya moja kwa moja michakato ya chaguzi katika nchi mbalimbali duniani ikiwemo kuingilia chaguzi za Russia na Iran.

Rais Joe Biden wa Marekani 

Pavel Sharikov mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Russia anasema: "Sababu iliyopelekea kuharibika uhusiano wa pande mbili kati ya Marekani na Russia ni kwamba kadhia ya Russia imekuwa mada na suala linalotumiwa kwa ajili ya ushindani wa kisiasa ndani ya Marekani."   

Utendaji wa Marekani kuhusu Iran baada ya Vita vya Pili vya Duna unaonyesha kuwa, nchi hiyo pamoja na Uingereza zilikuwa na nafasi ya moja kwa moja katika mapinduzi ya mwaka 1953 dhidi ya serikali ya kitaifa ya Mohammad Mosaddegh Waziri Mkuu wa wakati huo wa Iran. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu Marekani pia imekuwa ikiwachochea wananchi wa Iran wasishiriki katika uchaguzi na kisha kuhoji na kupinga matokeo  ya uchaguzi hususan uchaguzi wa Rais wa mwaka 2009 katika fremu ya vita vyake vya kipropaganda na vyombo vya habari. Si hayo tu bali hata hivi sasa pia Washington ilijaribu kuingilia uchaguzi wa karibuni wa Rais na wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran ili kupunguza ushiriki wa wananchi katika chaguzi hizo. 

Matukio yote haya yanaonyesha kuwa, Marekani inafanya chokochoko zote hizo huku yenyewe ikiwa na rekodi mbaya ya kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine hususan baada ya Vita vya Pili vya Dunia na kutoa tuhuma dhidi ya nchi mahasimu na wapinzani wake kuwa zinaingilia siasa za ndani za Marekani.  

Tags