Nov 21, 2021 11:34 UTC
  • Jeshi la Majini la Iran limetoa vipigo 6 ndani ya miezi 18 dhidi ya Marekani

Kamanda wa Kikosi cha Majini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema jeshi hilo la Iran limetoa pigo mara sita dhidi ya Wamarekani katika Ghuba ya Uajemi katika kipindi cha miezi 18 iliyopita.

Admeri Alireza Tangsiri amesema hayo katika mkutano wa wanafunzi mabasiji (wa kujitolea) wa Kiirani katika eneo ambalo ulikuwa ubalozi wa Marekani hapa Tehran, akiashiria kipindi cha mwaka mmoja na nusu tangu alipouawa Shahidi Luteni Jenerali Qassem Soleimani, aliyekuwa Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la SEPAH.

Admeri Tangsiri amesema vijana wa Iran wanapaswa kufahamu umuhimu wa eneo la Ghuba ya Uajemi, na ukweli kwamba nchi hii ina umuhimu na nafasi kubwa ya kijiografia katika eneo la Asia Magharibi.

Moja ya manowari za kijeshi za Iran

Ameeleza bayana kuwa, "Umuhimu huu umetufanya kutoa vipigo mara sita ndani ya mwaka mmoja na nusu katika makabiliano (dhidi ya Marekani), na aghalabu ya mapambano hayo hayakuakisiwa na vyombo vya habari."

Kamanda wa Kikosi cha Majini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ameashiria hatua ya mwezi uliopita ya Jeshi la SEPAH kufanikiwa kuzima uharamia wa jeshi la Marekani katika Bahari ya Oman na kueleza kuwa, hayo yalikuwa makabiliano ya pili, na kwamba makabiliano ya kwanza hayakuakisiwa na vyombo vya habari.

 

 

Tags