Nov 23, 2021 02:40 UTC
  • Safari ya Grossi Tehran; sisitizo la ushirikiano baina ya Iran na IAEA katika nyanja mbalimbali

Rafael Grossi Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia (IAEA) jana Jumatatu aliwasili hapa Tehran kwa lengo la kukutana na kufanya mazungumzo na Muhammad Eslami Mkuu wa Shirika la Atomiki la Iran na kuchunguza hali ya ushirikiano wa kiufundi wa pande mbili.

Kabla ya ziara hii Mkurugenzi Mkuu wa IAEA alikuwa amefanya ziara nyingine pia hapa Tehran kwa madhumuni ya kuimarisha ushirikiano kati ya Iran na wakala huo katika nyuga mbalimbali na pia kujadiliana kuhusu masuala ya kiufundi. Safari na ziara zote  hizo zina umuhimu katika kuendeleza ushirikiano na pia kufuatilia kadhia mbalimbali za pande mbili katika anga iliyo bora. Ndio maana Iran na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Nyuklia zikasisitiza kuendeleza mazungumzo kati ya pande mbili.  

Ziara ya huko nyuma ya Rafael Grossi hapa Tehran 

Kile kilicho muhimu kwa Iran ni kuona Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki ukifanya kazi kwa mujibu wa misingi mitatu mikuu yaani kutoegemea upande wowote, kuwa huru na kufanya kazi kwa kuzingatia taaluma.

Rafael Grossi Mkurugenzi Mkuu wa IAEA hivi karibuni aliwasilisha ripoti kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran; ripoti ambayo hata hivyo ilichanganyika na madai ya uwongo na yasiyo na msingi wowote dhidi ya Tehran. Kutolewa ripoti kama hiyo kwa kuzingatia rekodi ya mashinikizo ya kisiasa dhidi ya wakala huo si jambo jipya. Huko nyuma wakala huo pia ulijiweka mbali na mchakato wa kiufundi katika baadhi ya ripoti zake na kuzidisha masuala ya kisiasa katika utendaji wake jambo ambalo ni kinyume na msingi wa kuwa huru katika utendaji wa taasisi hiyo ya kimataifa.

Marekani inautumia kama wenzo wakala wa IAEA ili kuzidisha mashinikio katika kukaribia kuanza mazungumzo huko Vienna ya kuiondolea Iran vikwazo. Marekani inajaribu kila iwezalo kupitia wenzo wa vikwazo ili ione kama itafanikiwa kuilazimisha Iran ilegeze  misimamo yake mkabala wa kuiondolea vikwazo. Katika uwanja huo Marekani imejaribu mara kadhaa kutumia kama wenzo suala la uchunguzi wa wakala wa IAEA kuhusu Iran ili kuyatoa itibari mapatano ya JCPOA na wakati huo huo kuhalalisha siasa zake eti za mashinikizo ya kiwango cha juu dhidi ya Tehran; hata hivyo imegonga mwamba katika uwanja huo. 

Iran ni kati ya nchi wanachama zilizo bega kwa bega kwa kiasi kikubwa na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na wakati huo huo imetoa ushirikiano mkubwa sana kwa taasisi hiyo hadi sasa katika kuweka wazi shughuli zake za nyuklia zenye malengo ya amani. Wakati huo huo Iran siku zote imekuwa ikipendekeza kwa wakala huo njia ya kushirikiana pande mbili katika masuala ya kiufundi na kitaalamu kwa kuzingatia kuwa moja ya  malengo ya Marekani ni kuibua hali ya kutoaminiana kati ya Iran na IAEA. 

Kwa kuzingatia masuala hayo hapa kuna nukta mbili zinazopaswa kutiliwa maanani katika kuchambua safari ya Grossi mjini Tehran. Ya kwanza ni hii kuwa: Kwa kuzingatia msimamo wa Iran kuhusu mapatano ya kimataifa ya JCPOA na yale yaliyoafikiwa katika ziara za huko nyuma za Grossi hapa Tehran, Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) umefikia natija kwamba: Iran haiko tayari kufumbia macho haki zake; na wakati huo huo nchi kama China na Russia pia zinasisitiza juu ya uhalali wa takwa la Iran kwa mapatano ya JCPOA. 

Mapatano ya kimataifa ya JCPOA yaliyopasishwa na Baraza la Usalama la UN 

Kelsey Davenport Mkurugenzi wa Sera ya Udhibiti Silaha katika Taasisi Inayopiga Marufuku Silaha za Nyuklia ya mjini Washington anaamini kuwa: Hatua ya Iran ya kufungamana na kutekeleza majukumu yake kwa mujibu wa kanuni na miongozo ya IAEA imesaidia jitihada za serikali mbalimbali za kukabiliana na mashinikizo ya Marekani ya kutekelezwa vikwazo dhidi ya Iran.   

Nukta ya pili ni  sisitizo la Iran la kushirikiana katika hali ya kawaida na wakala wa IAEA katika masuala ya kiufundi; japokuwa Iran mara kwa mara imekuwa ikikosoa utendaji wa IAEA katika uwanja huo. Kwa hiyo katika uchambuzi wa mwisho tunaweza kusema kuwa safari ya Grossi Tehran ina lengo kuu na muhimu;  nalo ni sisitizo juu ya ulazima wa kuhitimishwa hatua na maamuzi ya kisiasa na yale yaliyo kinyume na sheria na wakati huo huo IAEA inapasa kutekeleza majukumu yake bila ya kuegemea upande wowote mkabala wa haki halali za Iran katika miradi yake ya nyuklia yenye malengo ya amani.