Nov 23, 2021 07:33 UTC
  • Iran: Marekani haina chaguo jingine isipokuwa kukubali uhalisia wa mambo

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ambaye anaongoza timu ya mazungumzo ya Jamhuri ya Kiislamu na kundi la 4+1 yatakayoanza Novemba 29 huko Vienna amesema kuwa, Marekani sharti ikubali hali halisi ya mambo kwa kufungamana na ahadi ilizotoa katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Ali Bagheri-Kani ameyasema hayo katika mahojiano na kanali ya televisheni ya al-Jazeera ya Qatar na kufafanua kuwa, "Marekani na Umoja wa Ulaya zinapaswa zinapaswa kuonesha kuwa zina irada ya kisiasa ya kutekeleza yale ziliyoyaafikia mwaka 2015."

Bagheri-Kani ameeleza bayana kuwa, nchi hizo za Magharibi zinapaswa kujiepusha na mashinikizo ya ndani ya nchi na badala yake zihakikishe kuwa mgogoro uliopo kuhusu JCPOA unapatiwa ufumbuzi.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameongeza kuwa, mafanikio ya mazungumzo hayo ya Vienna yatategemea irada ya upande wa pili na utayarifu wa kuliondolewa vikwazo vya kidhalimu taifa la Iran.

Kuondolewa vikwazo, lengo la vikao vipya Vienna

Wajumbe wa Iran na nchi za 4+1 ambazo ni China Russia, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani pamoja na mwakilishi wa Umoja wa Ulaya wanatazamiwa kukutana Vienna, Austria Novemba 29 kwa ajili ya duru ya saba ya mazungumzo.

Ikumbukwe kuwa, mazungumzo hayo yalisitishwa Juni wakati wa uchaguzi wa Iran na sasa baada ya serikali mpya ya Iran kutathmini hali ya mambo, mazungumzo hayo sasa yanatarajiwa kuanza upya.

Tags