Nov 25, 2021 14:34 UTC
  • Iran  yampongeza Katibu Mkuu mpya wa OIC kwa kuanza kazi rasmi

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amemtumia salamu za pongezi balozi Hussein Ibrahim Taha, Katibu Mkuu mpya wa Jumuiya ya Uushirikiano wa Kiislamu (OIC) kwa kuanza rasmi kazi yake na kueleza utayarifu wa Tehran kwa kushirikiana naye.

Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kumpongeza kiongozi huyo mpya wa OIC amesema kuwa, ana matumaini atatumia uwezo wa jumuiya hiyo muhimu ya Kiislamu kwa kukabiliana na mwenendo wa kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa kizayuni wa Israel.

Amesisitiza kuwa, kuhusiana na kadhia ya Palestina na kukabiliana na hujuma na uvamizi wa utawala haramu wa Israel sambamba na uporaji wake wa mali na miliki za Wapalestina kuna ulazima wa kutumiwa uwezo wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kwa ajili ya kukabiliana na mwenendo mbaya na usiofaa wa kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu.

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC)

 

Khatibzadeh ameongeza kuwa, kwa kuzingatia uwezo mkubwa OIC ulionao kwa ajili ya kuleta umoja katika umma wa Kiislamu na misingi na thamani asili na aali za Uislamu, Iran ina matumaini kwamba, duru mpya ya uongozi wa Katibu Mkuu wa OIC itaambatana kuongezeka juhudi za kudhaminiwa maslahi ya pamoja ya Umma wa Kiislamu.

Mwanadiplomasia mwandamizi Hussein Ibrahim Taha ambaye ni raia wa Chad alichaguliwa kuchukua wadhifa huo  Novemba mwaka jana katika Kikao cha 47 cha Baraza la Mawaziri wa OIC kilichofanyika Niamey nchini Niger na wiki iliyopita alianza rasmi kazi kama Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiisalmu (OIC) akimrithi Yusuf al-Uthaimeen aliyemaliza muda wake.

Tags