Nov 26, 2021 02:49 UTC
  • Iran yatoa majibu makali kwa bwabwaja mpya za utawala wa Kizayuni wa Israel

Msimamiaji wa nafasi ya uwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Vienna Austria ametoa majibu makali kwa bwabwaja na upayukaji mpya wa mwakilishi wa utawala wa Kizayuni wa Israel.

Shirika la habari la FARS limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, wakati wa kikao cha Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki kilichozungumzia mapatano ya nyuklia ya JCPOA, mwakilishi wa utawala wa Kizayuni alitoa madai yasiyo na msingi dhidi ya Iran lakini amepewa majibu makali na msimamiaji wa nafasi ya uwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Vienna, Bw. Mohammad Reza Ghaebi. 

Bw. Ghaebi amesema, hii si mara ya kwanza kwa mwakilishi wa utawala dhalimu wa Israel kuzusha maneno ya uongo kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran ambayo kila mtu anakiri ni ya amani kikamilifu.

kiwanda kichakavu cha nyuklia cha Dimona cha utawala wa Kizayuni

 

Ameongeza kuwa, kichekesho kikubwa ni kwamba, mwakilishi wa Israel anajipa uthubutu wa kutoa madai hayo ya uongo na kuzungumzia miradi ya nyuklia ya Iran ambayo iko chini ya uangalizi kamili wa IAEA wakati ambapo Israel haijawahi hata mara moja kuruhusu kukaguliwa miradi yake ya kutengeneza silaha za nyuklia.

IAEA imetoa ripoti chungu nzima zinazothibitisha kwamba miradi ya nyuklia ya Iran si ya kutengeneza kabisa silaha za nyuklia bali ni ya amani kikamilifu lakini utawala wa Kizayuni hadi hivi sasa unaendelea kufanya ukaidi wa hata kujiunga na Mkataba wa Kuzuia Uzalishaji na Uenezaji wa Silaha za Nyuklia NPT.

Bw. Ghaebi aidha amesema, Israel inaeneza maneno hayo ya uongo ili kuficha jinai zake za kushambuliwa kigaidi taasisi za nyuklia za Iran na wanasayansi wa nyuklia wa taifa hili la Kiislamu.

Tags