Nov 26, 2021 03:49 UTC
  • Khatibzadeh: Marekani na Troika ya Ulaya zinatoa taarifa za kilaghai na kiudanganyifu

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amekosoa vikali mienendo isiyo ya sawa ambayo Wamagharibi wamekuwa wakionyesha sambamba na kukaribia kuanza mazungumzo ya Vienna ya kujadili makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Katika ujumbe alioandika kwenye mtandao wa kijamii wa twitter katika kulinganisha muelekeo na hatua ilizochukua Marekani, Troika ya Ulaya na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati wa kukaribia kuanza mazungumzo ya Vienna, Saeed Khatibzadeh amesema: "Wakati wa kukaribia mazungumzo ya Vienna, pande za Magharibi zimechukua hatua ya kuongeza vikwazo, kutoa taarifa za kiudanganyifu, kueleza simulizi za upotoshaji na vilevile kunyamazia vitisho vya Israel. Na hii ni katika hali ambayo Iran imeunda timu makini na ya ngazi za juu ya mazungumzo na inataka kufikia makubaliano mazuri na ya haraka, kutekelezwa kikamilifu JCPOA na azimio nambari 2231 na inafanya mashauriano ya kikanda."

Khatibzadeh amekosoa mienendo isiyo ya sawa ya Wamagharibi wakati wa kukaribia kufanyika mazungumzo ya Vienna na akaongezea kwa kusema: "Inatosha ulinganishe vipaumbele tu vya pande mbili".

Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran ametoa kauli hiyo kufuatia hatua haribifu iliyochukuliwa na nchi tatu za Ujerumani, Ufaransa na Uingereza zinazounda Troika ya Ulaya, ambazo katika kikao cha jana cha Bodi ya Magavana ya Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki IAEA na kwa ajili ya kuifurahisha Marekani zilitoa taarifa ya kuituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba haitoi ushirikiano kamili kwa wakala wa IAEA. Na hii ni katika hali ambayo Tehran inashirikiana na wakala huo wa nishati ya atomiki katika ngazi na kiwango cha juu kabisa.../