Nov 29, 2021 03:19 UTC
  • Iran na Mali zatia saini mapatano ya ushirikiano katika madini

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Mali zimetiliana saini mapatano ya ushirikiano katika sekta ya uchimbaji madini. Mapatano hayo ni kati ya Shirika la Uhandisi wa Madini la Iran na Idara ya Uchimbaji Madini Mali.

Akizungumza mjini Tehran wakati wa utiwaji saini mapatano hayo, Taqi Nabi  Mkuu Shirika la Uhandisi wa Madini amesema shirika lake lina uwezo wa kushirikina na Mali katika nyuga za utafutaji, uchimbaji na usafishaji madini. Hali kadhalika amesema pande mbili zinaweza kubadilishana wataalamu na wanafunzi wa sekta ya madini na pia kushirikiana katika uwekezaji.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Uchimbaji Madini Mali Puna Abdul Ayah amesema nchi yake iko tayari kushirikiana na Iran katika sekta ya madini.

Amesema pande mbili zinaweza kubadilishana wataalamu na uzoefu kupitia kutembeleana, warsha na maonyesho ya sekta hii nchini Mali na Iran.

Aidha amesema Mali ni nchi yenye utajiri mkubwa wa madini ya dhahabu ambapo kila mwaka tani 50-62 huchimbwa kitaalamu katika migodi 14 nchini humo ambapo asilimi 66 huuzwa nje ya nchi.  Amesema dhahabu huchangia asilimia 10 ya Pato Ghafi la Taifa, GDP na asilimia 25 ya bajeti ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika. Abdul Ayah amesema asilimia 25 hadi 30 ya dhahabu nchini Mali huchimbwa kwa njia za kienyeji. Mbali na dhahabu amesema Mali ina utajiri mkubwa wa madini ya bauxite, urani na magnesium na hivyo nchi yake inaweza kushirikiana na Iran ili iweze kunufaika na utajiri wake wa madini.

Mali ni nchi yenye utajiri mkubwa wa madini ambao umekuwa ukiporwa kwa muda mrefu madola ya kikoloni hasa Ufaransa ambayo iliikoloni nchi hiyo.

 

Tags