Nov 29, 2021 03:24 UTC
  • Iran na Zimbabwe zajadili njia za kukabiliana na vikwazo vya Marekani

Maafisa wa ngazi za juu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Zimbabwe wamekutana mjini Tehran kujadili njia za kukabiliana na vikwazo vya Marekani katika sekta ya biashara.

Kikao hicho cha ushirikiano wa kiuchumi kimefanyika Jumapili chini ya uwenyekiti wa Mkurugenzi Mkuu wa Masuala ya Kimataifa katika Wizara ya Leba ya Iran Hamed Forouzan na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Zimbabwe katika masuala ya biashara ya kimataifa David Musabayana.

Katika kikao hicho, pande mbili zimejadili njia za kupanua uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kwa kuzingatia njia za kusambaratisha vikwazo vya Marekani ambavyo vinalenga nchi hizi mbili. Aidha kikao hicho kimefanyika kwa lengo la kutayarisha Mkutano wa Tisa wa Kamati ya Pamoja ya Kiuchumi ya nchi mbili.

Akizungumza katika kikao hicho, Fourouzan amesema Iran na Zimbabwe zina uhusiano wa muda mrefu na wa kina katika sekta za kisiasa na kiuchumi huku akisisitiza kuwa, daima Iran imekuwa muungaji mkono wa nchi zinazopinga ubeberu barani Afrika.

Amesema  kufanyika kikao kama hicho ni ishara ya azma imara ya Iran ya kushirikiana kibiashara na kiuchumi na Zimbabwe kwa lengo la kukabiliana na vikwazo vya kidhalimu ambavyo vimewekwa dhidi ya nchi hizo mbili.

Kwa upande wake, Musabayana amesema Zimbabwe ina azma imara ya kuimarisha uhusiano na Iran  na kuongeza kuwa,  'tutashirikiana ili tusambaratishe vikwazo vya Marekani."

 

 

Tags