Nov 29, 2021 14:01 UTC
  • Khatibzadeh: Iran inafanya juhudi zote ili kujidhaminia usalama wake

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, Tehran inafanya kila iwezalo kuhakikisha kuwa, inajidhamia usalama wake.

Saeed Khatibzadeh amesema hayo leo katika mkutano wake wa kila wiki na waandishi wa habari wa ndani na wa nje ambapo akijibu madai ya hivi karibuni ya utawala haramu wa Kizayuni wa Israel kwamba Iran, inatumia miji ya bandari ya Qeshm na Chabahar kwa ajili ya kufanya hujuma na mashambulio ya ndege zisizo na rubani amesema kuwa,  hakuna mtu anayeweza kutia dosari usalama wa Iran, jiografia ya Ghuba ya Uajemi na usalama unaohusiana na hayo.

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, madai hayo ya utawala haramu wa Israel hayana maana na kwamba, Tehran inaweza kufanya lolote lile kwa ajili ya kujidhaminia usalama wake.

Khatibzadeh sambamba na kutoa mkono wa kheri kwa mnasaba wa Siku ya Kimataifa ya Kuonesha Mshikamano na Taifa la Palestina amesema kuwa, Palestina kwa Iran ni malengo matukufu yasiyowezekana kutiwa dosari na kwamba, mateso na masaibu ya wananchi wa Palestina katu hayawezi kufutika katika fikra na akili za wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. 

 

Aidha amesema, utawala haramu wa Israel ungali unakanyanga na kukiuka haki za wananchi wa Palestina na kueleza kwamba, Iran sambamba na kuunga mkono haki za wananchi wa Palestina inalaani pia hatua ya baadhi ya mataifa ya Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala huo ghasibu kwani malengo ya Palestina siyo kitu cha kusahaulika.