Dec 02, 2021 02:58 UTC
  • Wamagharibi walivyohusika katika shambulio la silaha za kemikali lililofanywa Sardasht na utawala wa Saddam

Jumuiya ya kutetea waathirika wa ugaidi imesema, Sardasht ni nembo ya haki za binadamu duniani na imesisitiza kuwa: lazima watu wote, taasisi na serikali zilizoshirikiana na utawala wa Saddam katika kutenda jinai kubwa zaidi ya utumiaji wa silaha za kemikali dhidi ya binadamu wakemewe na kusailiwa.

Jumuiya hiyo ya kutetea waathirika wa ugaidi imeeleza katika taarifa kwamba, kushambuliwa eneo la Sardasht kwa silaha za kemikali kunakumbusha zama za ushenzi za Enzi ya Kati, yaani Middle Ages katika enzi hizi za kustawi kwa ustaarabu wa mwanadamu na ikabainisha kuwa, tarehe 30 Novemba, ambayo ni Siku ya Kimataifa ya kuwakumbuka waathirika wote wa silaha za kemikali ni fursa ya kuwataja na kuwaenzi walioumizwa na kudhuriwa kwa silaha za kemikali, sambamba na kuwataka viongozi wa dunia na asasi za kimataifa na hasa Umoja wa Mataifa wachukue hatua athirifu na zuilifu kwa kutekeleza ahadi na wajibu wao kama ilivyoainishwa kwenye Hati ya Umoja wa Mataifa na nyaraka nyingine za kimataifa kuhusiana na majeruhi na waathirika wa silaha za kemikali.

Baadhi ya majeruhi wa silaha za kemikali za utawala wa dikteta Saddam

Tarehe 28 Juni, 1987 utawala wa Baath wa Iraq ulitumia mabomu ya kemikali kushambulia maeneo manne ya mji wa Sardasht yaliyokuwa na msongamano wa watu. Katika shambulio hilo la kinyama, wakazi 110 wa mji huo waliuawa shahidi na wengine 8,000 waliathirika kwa gesi ya sumu ya silaha hizo.

Wakati vita vya miaka minane vya kulazimishwa, vilivyoanzishwa na utawala wa Baath wa Iraq vilipokuwa vimeshtadi, mji wa mpakani wa Sardasht uligeuzwa kuwa mji wa kwanza kushambuliwa, tena mara nne mtawalia, kwa silaha za kemikali duniani tangu baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia na kupitishwa mikataba ya kupiga marufuku matumizi ya silaha za kemikali.

Utumiaji wa silaha za kemikali umepigwa marufuku kulingana na mikataba ya makubaliano ya kimataifa. Kwa mujibu wa hati zilizopitishwa kwenye mkutano wa suluhu wa The Hague wa mwaka 1899 na 1907, kifungu cha 6 cha hati kuu ya mahakama ya Nuremberg ya mwaka 1964, kifungu cha 5 cha hati ya makubaliano ya Washington ya mwaka 1922, kifungu cha 3 cha Azimio la Dunia la Haki za Binadamu la mwaka 1948 pamoja maazimio ya mkutano wa kupiga marufuku silaha za kemikali, ni marufuku kutumia silaha hizo.

Miongoni mwa athari za gesi ya mvuke wa sumu

Kimya cha Jumuiya za Kimataifa kuhusiana na jinai hiyo kimetokana na nchi za Ulaya na Marekani kuchangia katika kutokea kwa maafa hayo. Shambulio la silaha za kemikali lililofanywa na utawala wa Baath wa Iraq dhidi ya wakazi wa mji wa Sardasht lilijiri miezi tisa baada ya Marekani kutumia kura yake ya turufu kuzima juhudi zilizofanywa na akthari ya wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa za kupitisha taarifa ya kuilaani Iraq kwa kutumia silaha za kemikali, huku Uingereza na Ufaransa zikiamua kutoshiriki katika zoezi la upigaji kura. Ukweli ni kwamba nchi za Magharibi, ambazo ndizo zilizoiuzia Iraq silaha za kemikali, si tu hazikuchukua hatua yoyote kuhusiana na jinai hiyo, lakini zilikwenda mbali zaidi kwa kuikanusha.

Nyaraka zilizotelewa zinaonyesha kuwa, serikali za Magharibi, ikiwemo ya wakati huo ya Marekani zilikuwa zikijua kwamba utawala wa Saddam unatumia aina mbalimbali za silaha za kemikali katika vita dhidi ya Iran, zikiwemo za gesi ya Sarini, gesi ya neva na sumu ya mvuke, lakini ziliendelea kulipatia jeshi la Iraq misaada ya kiufundi ya kutengenezea silaha hizo.

Ripoti ya uchunguzi iliyotolewa Agosti 26, 2013 na jarida la Foreign Policy linalochapishwa nchini Marekani inaoneysha kuwa, kuanzia mwaka 1982, nchi hiyo ilikuwa na "ushahidi kamili" kwamba Iraq inatumia silaha za kemikali.

Dikteta Saddam, ambaye alisaidiwa kwa hali na mali na madola ya Magharibi katika vita dhidi ya Iran

Aidha gazeti la Washington Post liliwahi kutoa ripoti tarehe 30 Desemba 2002, miezi mitatu kabla ya Marekani kuishambulia na kuivamia kijeshi Iraq juu ya kuwepo nyaraka zinazoonyesha kuwa waliokuwa marais wa Marekani Ronald Reagan na George Bush baba waliafiki kuuziwa utawala wa Saddam "mada za kemikali za sumu na za virusi angamizi vya biolojia."

Ripoti mbalimbali zinaonyesha pia kuwa, kuna mashirika zaidi ya 400 yanayozalisha mada za kemikali, ambayo mengi yao ni ya Ujerumani na Uingereza, ambayo yalichangia katika kuuzatiti utawala wa Baath wa Iraq kwa silaha za kemikali.

Shambulio la silaha za kemikali dhidi ya Sardasht ni dhihirisho la ukiukaji wa kutisha na angamizi wa haki za binadamu uliofanywa na Marekani na waitifaki wake wa Magharibi. Na kwa sababu hiyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hadi sasa imeshafungua mashtaka katika mahakama za kimataifa dhidi ya mashirika kadhaa ya Magharibi, ambayo wakati wa vita vilivyoanzishwa na utawala wa Baath dhidi yake, yaliupatia utawala huo mada za kemikali za kutengenezea silaha hizo angamizi. 

Raia wasio na hatia wakiwemo watoto waliouawa kwa silaha za kemikali ulizopatiwa utawala wa Saddam na Ujerumani

Matarajio yaliyopo ni kuziona asasi za kimataifa kama Umoja wa Mataifa ukichukua hatua kwa ajili ya kutekeleza ahadi na majukumu yake kuhusiana na suala hilo, ambapo mbali na kuwabebesha dhima ya jinai hiyo nchi zilizoshirikiana na utawala wa Baath wa Iraq, kuhakikisha pia kwamba jinai za aina hiyo hazirudiwi tena.../