Dec 02, 2021 03:01 UTC
  • Austria: Tunafanya juhudi ili kufikiwe makubaliano ya nyuklia na Iran

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Austria imesema katika taarifa yake kuwa, nchi hiyo ambayo ni mwenyeji wa duru nyingine ya mazungumzo ya nyuklia inaunga mkono juhudi za pande zote katika mazungumzo hayo ili kuhakikisha kunafikiwa makubaliano.

Katika ujumbe wake katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Austria imeashiria mazungumzo ya Michael Linhart Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa nchi hiyo na Ali Bagheri, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Iran anayehusika na masuala ya kisiasa na kueleza kwamba, nchi hiyo inafanya kila iwezalo ili pande husika zifikie makubaliano kuhusiana na kutekelezwa kikamilifu makubaliano ya nyuklia ya JCPOA.

Sehemu nyingine ya taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Austria imebainisha kuwa: Mazungumzo baina ya Michael Lihart na Ali Bagheri yamekwenda vizuri.

Duru mpya ya mazungumzo ya nyuklia ya Iran na kundi la 4+1 ilianza Jumatatu ya wiki hii huko Vienna mji mkuu wa Austria.

 

Nchi zinaounda kundi la 4+1 ni China, Russia, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani pamoja na mwakilishi wa Umoja wa Ulaya. Mazungumzo hayo yameanza baada ya kusimama kwa takribani miezi mitano.

Ujumbe wa Iran katika mazungumzo hayo unaongozwa na Ali Bagheri, Naibu Waziri wa Mashauri ya Kigeni anayeshughulikia masuala ya kisiasa ambaye anaongoza ujumbe wa  wataalamu wa masuala ya sheria, benki na nishati kwa ajili ya kushiriki katika mazungumzo hayo.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imesisitiza mara chungu nzima kabla ya kuanza duru hii ya mazungumza kwamba, inachotaka ni kuondolewa vikwazo vyote vya kidhulma na vya upande mmoja vilivyowekewa taifa hili.