Dec 02, 2021 12:19 UTC
  • Bagheri: Iran imewasilisha matini ya pendekezo lake kwa kundi la 4+1

Mkuu wa Timu ya Iran katika Mazungumzo ya Kuondoa Vikwazo vya Kidhalimu dhidi ya Iran na ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayeshughulikia masuala ya kisiasa amesema Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewaslisha matini ya pendekezo lake kwa kundi la 4+1.

Ali Bagheri Khani Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayeshughulikia masuala ya kisiasa na Mkuu wa Timu ya Iran katika Mazungumzo ya Kuondoa Vikwazo vya Kidhalimu dhidi ya Iran ameongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imewasilisha kwa kundi la 4+1 katika mazungumzo ya Vienna matini ya pendekezo lake katika kalibu ya masuala mawili ambapo moja ni kuhusu kuondolewa vikwazo vya kidhalimu na lingine kuhusiana na masuala ya nyuklia. Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayehusika na masuala ya kisiasa awali alieleza kuwa: Iran imedhamiria kwa dhati kufanya mazungumzo na ipo tayari kivitendo kwa lengo la kufikia mapatano.  

Jopo kazi la kuondoa vikwazo vya kidhalimu na vilivyo kinyume cha sheria vya Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia tayari limeanza shughuli zake huko Vienna, Austria kwa kuwashirikisha wataalamu bora wa Kiirani na wa pande nyingine ndani ya mapatano ya JCPOA. 

Wanadiplomasia wa ngazi ya juu wa kundi la 4+1, Umoja wa Ulaya na wawakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Jumatatu wiki hii walisisitiza kuwa upande wa Iran umekubaliana kwamba suala la kuondoa vikwazo vya kidhalimu na haramu vya Marekani dhidi ya Iran lifuatiliwe kwa uzito maalumu. 

Kundi la 4+1 

Kwa mujibu wa mazungumzo yaliyofanyika hadi sasa, jopo kazi jingine kuhusu masuala ya nyuklia pia linatazamiwa kuundwa hata hivyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatilia mkazo udharura wa kuwekwa katika ajenda ya kikao cha mazungumzo huko Vienna suala la kuondolewa vikwazo.