Dec 03, 2021 04:47 UTC
  • Kamanda wa IRGC: Marekani iondoke karibu na ardhi ya Iran

Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) ameitaka Marekani iviondoe vikosi vyake katika maeneo yanayopakana na Jamhuri ya Kiislamu, kabla hawajafikiwa na hatima kama waliyopata huko Afghanistan.

Brigedia Jenerali Esmaeel Qa'ani alisema hayo jana Alkhamisi katika hafla iliyofanyika katika mkoa wa Fars, kusini magharibi mwa Iran na kuongeza kuwa, "tunawaambia Wamarekani kwamba bado mna muda wa kuondoka katika maeneo yetu ya kijiografia kwa idhilali, vinginevyo mtatimuliwa katika eneo hili kwa madhila zaidi ya mlivyoshuhudia Afghanistan."

Amewahutubu Wamarekani kwa kuwaambia: Hamutoendelea kufanya yale mumekuwa mukifanya huko nyuma. Mbinu ya kushambulia na kukimbia haifanyi kazi tena.

Brigedia Jenerali Esmaeel Qa'ani amebainisha kuwa, Marekani imepigana vita nchini Afghanistan kwa muda wa miaka 20 lakini hawakupata chochote. 

Mji wa makombora ya IRGC ya Iran

Amefafanua kwa kusema, Wamarekani wamekuwa wakianzisha vita katika maeneo mbalimbali duniani, na kuvuna faida kwa kuuza silaha, lakini walivamia Iraq na Afghanistan bila mualiko, na hatimaye wakaondoka mikono mitupu baada ya miaka 20.

Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la SEPAH ameongeza kuwa, vikwazo na vitisho vya Marekani dhidi ya taifa la Iran vimeshindwa kuzaa matunda.

 

 

  

Tags