Dec 05, 2021 14:54 UTC
  • Iran: Hatutalegeza kamba katika kushinikiza kuondolewa vikwazo haramu

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran anayeshughulikia masuala ya kisiasa amesema Jamhuri ya Kiislamu katu haitolegeza kamba katika mazungumzo ya Vienna, Austria na itaendelea kushinikiza kuondolewa vikwazo vya kidhalimu na vilivyo kinyume cha sheria vya Marekani dhidi ya taifa hili.

Ali Baqeri-Kani ambaye anaongoza timu ya Iran katika Mazungumzo ya Kuondoa Vikwazo vya Kidhalimu dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu huko Vienna amesema hayo katika mahojiano na shirika la habari la Italia, ANSA na kuongeza kuwa, Marekani ndiyo iliyochukua hatua ya kujiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA, na kwa msingi huo, ndiyo inayopaswa kuchukua hatua ya kwanza hivi sasa.

Mwanadiplomasia huyo wa ngazi ya juu wa Iran ameeleza bayana kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ina imani na mazungumzo yanayoendelea, na inaitakidi kuwa mazungumzo hayo yatazaa matunda.

Wanadiplomasia wa ngazi ya juu wa kundi la 4+1, Umoja wa Ulaya na wawakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Jumatatu wiki hii walisisitiza kuwa upande wa Iran umekubaliana kwamba suala la kuondoa vikwazo vya kidhalimu na haramu vya Marekani dhidi ya Iran lifuatiliwe kwa uzito maalumu.

 Wakati huohuo, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran anayeshughulikia masuala ya kisiasa ameiambia kanali ya televisheni ya al-Jazeera ya Qatar kuwa, Tehran itaendelea kufanya miradi yake ya nyuklia yenye malengo ya amani.

Ali Baqeri-Kani amesisitiza kuwa, mapendekezo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kundi la 4+1 katika mazungumzo ya Vienna hayawezi kukataliwa na madola makubwa ya dunia, kwa kuwa misingi yake ni vipengee vya mapatano ya JCPOA yaliyotiwa saini mwaka 2015 na madola hayo hayo.

Tags