Dec 06, 2021 09:01 UTC
  • Safari ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria mjini Tehran

Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria Faisal al Miqdad ambaye jana usiku aliwasili hapa mjini Tehran, leo Jumatatu, tarehe 6 Desemba amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Hossein Amir-Abdollahian, ambapo wawili hao wamejadili na kubadilishana mawazo juu ya masuala mbali mbali yanayohusu pande mbili.

Bashar al Jaafari, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria ameandamana na al Miqdad katika safari hiyo.

Malengo ya safari ya waziri wa mambo ya nje wa Syria mjini Tehran yamejikita katika kubadilishana mawazo juu ya masuala ya eneo, makubaliano ya kisiasa na kiuchumi yaliyofikiwa na nchi mbili na mashirikiano ya kistratejia yaliyoko baina yao.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Hossein Amir-Abdollahian (kulia) alipomlaki mgeni wake Faisal Miqdad, Waziri wa Mambo ya Nje wa Syria

Iran na Syria zimechukua hatua ambazo zimeziwezesha kupata ushindi wa pamoja katika medani za vita na mapambano dhidi ya ugaidi; na hivi sasa zinaandaa mpango wa kustawisha zaidi uhusiano wao katika kipindi cha kuikarabati na kuijenga upya Syria. Katika mazingira ya hivi sasa, kustawisha mashirikiano katika sekta za ufundi, nishati, bandari, uchukuzi na usafirishaji na vilevile kuharakisha utekelezaji wa makubaliano ya kibiashara na kibenki kwa madhumuni ya kukabiliana na vikwazo vya kidhulma dhidi ya nchi hizi mbili kuna umuhimu wa kistratejia. Kuhusiana na suala hilo, wiki iliyopita yalifanyika maonyesho maalumu ya kibiashara ya Iran mjini Damascus, Syria yaliyoshirikisha mashirika ya Kiirani yanayojihusisha na utengenezaji dawa, mashine, uundaji meli, utoaji huduma za maji, utengenezaji nguo, huduma za elektroniki, ufundi na uhandisi pamoja na mashirika ya ubunifu wa taaluma. Sambamba na kufanyika maonyesho hayo,  Reza Fatemi Amin, Waziri wa Viwanda, Madini na Biashara wa Iran alifanya ziara ya kuitembelea Syria.

Uhusiano wa Iran na Syria hivi sasa umestawi na ni wa nyuga mbalimbali; na kuna matarajio makubwa katika mustakabali ya kustawishwa zaidi uhusiano huo katika nyanja zote. Syria imeshaivuka awamu kuu ya vita vya mapigano vilivyoanzishwa dhidi ya nchi hiyo. Hata hivyo vita hivyo vimeisababishia hasara kubwa nchi hiyo. Baada ya kufifia moto wa vita na mgogoro, hivi sasa serikali ya Syria inahitaji msaada wa nchi rafiki na waitifaki kwa ajili ya kuijenga upya nchi hiyo.

Syria ilivyoharibiwa kwa vita

Syria, ambayo ni moja ya nchi muhimu na yenye mchango athirifu katika mhimili wa muqawama, kuanzia mwishoni mwa mwezi Januari 2011 ilitumbukizwa kwenye lindi la vita vya kulazimishwa vilivyoanzishwa na Wamagharibi na waitifaki wao wa eneo. Moja ya malengo ya kuibebesha Syria mzigo huo mzigo wa vita lilikuwa ni kuigawanya vipande vipande nchi hiyo. Hata hivyo njama hiyo iligonga mwamba kutokana na muqawama ulioonyeshwa dhidi ya mashinikizo ya adui. Ukweli ni kwamba, kitu kinachozielekeza sera za nje za Tehran na Damascus katika muelekeo mmoja hivi sasa ni azma ya nchi mbili ya kuendeleza vuguvugu la muqawama. Sifa hii ni moja ya mihimili mikuu katika sera za nje za Jamhrui ya Kiislamu ya Iran na Syria; na uimarishwaji wa uhusiano wa nchi mbili umesimama juu ya msingi na mhimili huo.

Kwa kufuata muelekeo huo na kwa kuzingatia upeo wa uhusiano wao, Tehran na Damascus zinaendelea kuimarisha na kustawisha uhusiano na ushirikiano wao. Kitu ambacho kimesaidia kuimarisha uhusiano huo na kuipa uthabiti misimamo ya nchi mbili ni hali ya kuaminiana iliyopo baina yao, jambo ambalo limeufanya uhusiano wa nchi mbili ufikie kiwango cha kistratejia katika nyanja za kisiasa, kiuchumi, kibiashara na katika kukabiliana na vitisho vya kiusalama. Iran na Syria zimekuwa bega kwa bega pale zilipohitaji kusaidiana; na hivi sasa, ambapo kipindi cha kuikarabati na kuijenga upya Syria kimeanza, Iran iko bega kwa bega pia na nchi hiyo.

Hassan Hanizadeh, mtaalamu wa masuala ya kisiasa anasema, kutokana na mtazamo huo, uhusiano wa Tehran na Damascus ni wa kistratejia. Sambamba na kuashiria kuwa hivi sasa Syria inaivuka awamu ya msukosuko mkubwa wa mgogoro wa miaka minane na kuingia kwenye awamu mpya ya ujenzi mpya wa nchi, Hanizadeh anaeleza kwamba, kutokana na tajiriba ya muda mrefu iliyopata Iran katika ukarabati wa miji yake iliyoharibiwa kwa vita, inaweza kuipatia serikali na wananchi wa Syria tajiriba yake hiyo katika uga huo. Lakini mbali na hilo, kushiriki Iran katika kipindi cha ukarabati na ujenzi mpya wa Syria kutawapatia fursa kadhaa wadau wake wa kiuchumi na kibiashara.

Waziri Hossein Amir-Abdollahian

Wakati Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alipofanya ziara hivi karibuni nchini Syria alisema, uhusiano wa Tehran na Damascus ni wa kistratejia na akabainisha kwamba, Syria imevuka kipindi kigumu; na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itakuwa na mchango hai na amilifu katika kipindi hiki cha kustawika zaidi uhusiano wa nchi mbili.../