Dec 06, 2021 13:05 UTC
  • Dakta Ibrahim Raeisi: Syria ipo mstari wa mbele katika kupambana na Wazayuni

Rais Ibrahim Raeisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo amekutana na kufanya mazungumzo hapa mjini Tehran na Faisal Mekdad, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Syria na kusema kuwa, nchi hiyo ya Kiarabu ipo mstari wa mbele katika mapambano na muqawama dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.

Rais wa Iran ameashiria katika mazungumzo hayo manufaa ya pamoja ya pande mbili, matukio ya kieneo na kimataifa na kusema kuwa,hii leo kuna haja ya kuandaliwa mipango ya muda mrefu na ya pande zote kwa ajili ya ustawi na kuimarishwa zaidi uhusiano wa Tehran na Damascus.

Rais Ibrahim Raeisi amesema pia kuwa, uwepo usio wa kisheria wa vikosi vya kigeni katika eneo na katika ardhi ya Syria ni jambo hatarishi kwa usalama na uthabiti wa eneo na kuongeza kuwa, kundi la kigaidi la Daesh limeanzishwa na kulelewa na Marekani, na hii leo uwepo wa Daesh na Washington katika eneo lolote lile katika ukanda huu kutauletea hasara kubwa usalama, uthabiti na amani ya mataifa ya eneo hili. 

Mazungumzo ya Rais wa Iran na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Syria

 

Kadhalika Rais Ibrahim Raesi amesistiza udharura wa kuheshimiwa mamlaka na ardhi yote ya Syria na kueleza kwamba, kupuuza hilo ni jambo ambalo halikubaliki kwa namna yoyote ile na bila shaka wananchi wa Syria katu hawawezi kulivumilia hilo.

Kwa upande wake, Faisal Mekdad, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Syria sambamba na kumkabidhi Rais wa Iran ujumbe kutoka kwa Rais Bashar al-Assad na kumwalika kuitembelea Syria amesema kuwa, Damascus imeazimia kwa dhati kutumia uwezo wake wote kwa ajili ya kuimarisha uhusiano wake na Tehran.