Dec 07, 2021 08:02 UTC
  • Hatua za Imarati za kuboresha uhusiano na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran

Jumatatu ya jana ya tarehe 6 Disemba, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) alifanya safari ya siku moja hapa mjini Tehran ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiwemo Rais Sayyid Ibrahim Raeisi na Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa.

Afisa huyo wa Imarati alipata fursa ya  kubadilisha mawazo na wenyeji wake kuhusiana na masuala mbalimbali yakiwemo ya uhusiano wa pande mbili na matukio ya kieneo na kimataifa. Rais Ibrahim Raeisi ameashiria katika mazunguzmo yake na Sheikh Tahnoun bin Zayed Al-Nahyan  kuhusu uhusiano wa kirafiki kati ya nchi mbili na kueleza kuwa, siasa za nje za serikali mpya ya Iran zinatoa kipaumbele kwa suala la kuwa na uhusiano mzuri na nchi za eneo hili, na ndio maana Tehran inakaribisha kwa mikono miwili juhudi za kustawishwa uhusiano kati yake na Imarati.  Kwa upande wake, Sheikh Tahnoun bin Zayed Al-Nahyan Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) amesema: Sisi sote ni watoto wa eneo hili na mustakabali wetu ni mmoja; kwa msingi huo kuimarishwa uhusiano wa nchi mbili ni suala lilnalopewa kipaumbele katika ajenda ya Abu Dhabi, na tupo tayari kustawisha ushirikiano na Iran."

Aidha katika mazungumzo yake na Admeri Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran , mshauri huyo wa usalama wa taifa wa Imarati amesema kwamba, Iran ni taifa kubwa na lenye nguvu Asia Magharibi ambalo lipo katika ukanda usio na mithili kijiopolotiki na njia kuu ya mawasiliano ya Mashariki na Magharibi mwa ulimwengu.

Hii ni safari ya kwanza ya afisa wa ngazi za juu wa Imarati katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran baada ya kuibuka hitilafu na mivutano katika uhusiano wa Tehran na mataifa ya Imarati na Saudi Arabia takribani miaka mitano iliyopita. Katika miezi ya hivi karibuni Imarati imefanya juhudi kubwa za kuzifanya siasa zake za kigeni kuwa na uwiano na kujikurubisha kwa waitifaki wa Iran ikiwemo Syria. Sheikh Abdullah bin Zayed al-Nahyan, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Umoja wa Falme za Kiarabu mwezi uliopita wa Novemba alifanya safari nchini Syria na kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Bashar al-Assad. Safari hiyo ilifanyika baada ya kupita miaka kumi baada ya kuvunjwa uhusiano wa kidiplomasia baina ya Abu Dhabi na Damascus kufuatia mgogoro wa Syria uliozuka mwaka 2011.

Admeri Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran akisalimiana na mgeni wake Sheikh Tahnoon bin Zayed Al Nahyan, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati)

 

Katika miezi ya hivi karibuni mwenendo wa ushirikiano wa Iran na Imarati unaonekana kuongezeka licha ya kuweko mafaili ya hitilafu katika uga wa kisiasa na kieneo. Hii ni ishara na ithbati tosha kwamba, mataifa haya mawili jirani yameazimia kwa dhati kuboresha uhusiano wao. Tehran na Abu Dhabu zimeazimia kuhakikisha kuwa, zinazuia kuongezeka mizozo na wakati huo huo kutumia vyema uwezo zilionazo nchi hizo hususan katika uwanja wa biashara na uchumi. Katika historia ya uhusiano mkongwe wa Iran na Imarati, mahusiano ya kiuchumi ni miongoni mwa mambo muhimu ambayo yamekuwa na mchango mkubwa katika kuleta mfungamano baina ya mataifa haya mawili.

Ni kwa muktadha huo, ndio maana hata katika mazingira mabaya kabisa ya vikwazo na kupungua kwa uhusiano wa kisiasa, Imarati imeendelea kuwa miongoni mwa nchi tano za awali ambazo ni washirika wa kibiashara wa Iran.

Sababu nyingine zenye taathira ambazo zinaonyesha udharura wa kuweko ushirikiano wa Imarati na Iran ni juhudi za kuhitimisha migogoro ya kiusalama katika jamii ya Kiislamu, ambayo akthari yake inasabishwa na ungiliaji wa madola ya kigeni kutoka nje ya eneo hili.

Mazungumzo ya Rais Ibrahim Raeisi na Sheikh Tahnoon bin Zayed Al Nahyan, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu {Tehran-06.12.2021}

 

Admeri Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran sambamba na kuashiria nukta hii katika mazungumzo yake na Sheikh Tahnoun bin Zayed Al-Nahyan, Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) alisisitiza kuwa, njia pekee ya kupatikana usalama na uthabiti wa kudumu wa eneo hili ni kuweko ushirikiano wa mataifa ya eneo hili.

Hapana shaka kuwa, maslahi ya Iran na Imarati katika uga wa kisiasa, kiuchumi na kiusalama zikiwa nchi mbili jirani yanahitajia kuboreshwa na kupanuliwa uhusiano wa pande mbili na kieneo. Lililo dhahir shahir ni kuwa, viongozi wa Tehran na Abu Dhabi wamefikia natija hii kwamba, wanapaswa kufanya juhudi za kuleta mabadiliko katika utendaji wao ili kuleta muelekeo wa pamoja wa kieneo.

Mohammad Mehdi Mazaheri, mweledi na mtaalamuu wa masuala ya kisiasa anasema kuhusiana na suala hilo kwamba: Imarati imefahamu wazi kuwa, hakuna tena himaya na uungaji mkono wa Marekani kama nguvu kutoka nje ya eneo hili; na ndio maana nayo kama ilivyo kwa mataifa mengine ya Kiarabu ya Ukanda wa Ghuba ya Uajemi inapaswa kutafuta mwarobaini wa kuratibu na kuboresha uhusiano wake na majirani zake.