Dec 20, 2021 02:31 UTC
  • Takwa la China la kuondolewa vikwazo vya Iran

Mwakilishi wa China katika kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ametaka kuondolewa vikwazo vya upande mmoja dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Geng Shuang amesema Marekani imekosea katika kuanzisha mgogoro wa nyuklia wa Iran na kuitaka Washington iondoe vikwazo vyake vya upande mmoja ili kuandaa mazingira ya kurejea katika mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kimefanyika huku mazungumzo ya Vienna kuhusu miradi ya nyuklia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pia yakiendelea. Kwa msingi huo, Marekani na nchi za Ulaya yaani Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zimefanya kila ziwezalo kuishinikiza Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ili ikubali matakwa yao kwa kulifikisha suala hilo mbele ya Baraza la Usalama  la UN. Hii ni kwa sababu ujumbe wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazungumzo ya Vienna hadi sasa umedhihirisha msimamo mkuu wa Tehran na hivyo kusambaratisha siasa na mipango ya Marekani ya kutaka kuvuruga mazungumzo ya Vienna. 

Folker Trier mchambuzi wa masuala ya kiuchumi wa Ujerumani anaamini kwamba: Trump alifanya kosa kubwa  kujitoa katika mapatano ya JCPOA kwa sababu  alizuia kutekelezwa kikamilifu mapatano hayo.

Uungaji mkono wa pande zote wa China na Russia kwa miradi ya nyuklia ya Iran; na ombi lao kwa Marekani la kuitaka iondoe vikwazo ilivyoiwekea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wakati wa utawala wa rais wa zamani wa nchi hiyo Donald Trump unaweza kuandaa uwanja wa kurejea Washington katika mapatano ya JCPOA. Hii ni kwa sababu, Trump alichukua na kutekeleza sera na maamuzi ya upande mmoja kwa kuathiriwa na siasa na matakwa ya utawala wa Kizayuni na kuiondoa Marekani katika mapatano ya kimataifa ya JCPOA na kisha kuirejeshea Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vikwazo vyote vilivyokuwa vimeondolewa baada ya kufikiwa mapatano ya nyuklia ya JCPOA. Si White House tu bali hata waitifaki wa Washington wenyewe wanaitaja hatua hiyo ya upande mmoja  ya Marekani kwamba ilikuwa makosa. 

Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump 

Taasisi moja ijulikanayo kwa jina la The Carnegie Endowment for International Peace ambayo inaungwa mkono na makumi ya wataalamu wa ngazi ya juu wa nchini Marekani inaamini kuwa hatua ya Marekani ya kujitoa kwa upande  moja katika mapatano ya JCPOA ni kosa kubwa na kusisitiza kuwa mapatano hayo ya nyuklia yalikuwa kiashiria kikuu cha hatua na ufanisi wa diplomasia kuhusu miradi ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya amani ambayo yaliharibiwa na Rais wa Marekani wa chama cha Republican.  

Mapatano ya nyuklia ya JCPOA 

Alaa kulli haal, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imeboresha ushirikiano wake na Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA) na kuonyesha kivitendo kuwa haina kadhia yoyote ya siri katika miradi yake ya nyuklia; na ndio maana Marekani na waitifaki wake wameshindwa kuitwisha Iran matakwa yao. Wakati huo huo China na Russia ambazo zina mgongano wa pamoja wa kimaslahi kati yao na Marekani katika masuala mbalimbali yakiwemo masuala ya uchumi na kadhia ya Ukraine zinatarajiwa kushikilia misimamo yao kwenye kikao cha Vienna katika kuunga mkono miradi ya nyuklia ya Iran yenye malengo ya amani na kutoiruhusu Marekani kutekeleza hatua hatari katika miradi hiyo ya nyuklia ya Iran, kupitia ubaguzi wa kinyuklia. Aidha makubaliano yaliyofikiwa hivi karibuni kati ya Marekani na Uingereza ya kuipatia Australia nyambizi za nyuklia; makubaliano ambayo yamelalamikiwa pia na China ni jambo jingine linalopasa kutiliwa maanani katika uwanja huo wa migongano ya kimaslahi na uwezekano mkubwa. 

Tags