Dec 25, 2021 09:01 UTC
  • Iran: Mazoezi ya kijeshi ya Mtume Mtukufu SAW 17 yana ujumbe wa udugu kwa nchi jirani

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema ujumbe wa mazoezi makubwa ya kijeshi ya Mtume Mtukufu SAW 17" ni udugu na usalama kwa nchi rafiki na jirani.

Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran aliyasema hayo Ijumaa ambapo, sambamba na kuambatanisha matamshi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu kuhusu vikosi vya kijeshi, ameashiria mazoezi makubwa ya kijeshi yaliyopewa jina la "Mtume Mtukufu SAW 17" ambayo yamefanyika wiki hii nchini Iran na kusema: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kama nchi yenye nguvu na uwezo daima imekuwa ikitoa wito wa amani na utulivu katika eneo la Magharibi mwa Asia." Ameongeza kuwa, Mazoezi ya Kijeshi ya "Mtume Mtukufu SAW 17", mbali na kuwa yanaonesha azma imara na isiyoterereka ya kulinda ardhi ya Kiislamu na kutoa jibu kali kwa maadui wa nchi hii, pia mazoezi hayo yana ujumbe wa udugu na usalama kwa nchi rafiki na jirani.

Siku ya Jumatatu jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran lilianza mazoezi ya pamoja yaliyopewa jina la "Mtume Mtukufu SAW 17" katika Ghuba ya Uajemi, Lango-Bahari la Hormuz na pwani ya mikoa ya Hormozgan, Bushehr na Khuzestan.

Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran

Mazoezi hayo ambayo yalimalizika Ijumaa yamefanyika kwa shabaha ya kukabiliana na vitisho vya aina mbalimbali vya adui. 

Kamanda wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu Meja Jenerali Hossein Salami amesema mazoezo hayo yana ujumbe wa wazi kwa utawala wa Kizayuni wa Israel. Ameongeza kuwa, ujumbe wa mazoezi hayo ni mzito kwa utawala wa Kizayuni kwamba unapaswa kuchukua tahadhari usifanye kosa lolote kwani ukiibua chokochoko basi mikono yake itakatwa.

Tags