Jan 06, 2022 02:50 UTC
  • Mahakama ya Iran yakosoa sera za kupenda vita za Wamagharibi

Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran amekosoa vikali sera za kupenda na kuchochea vita za nchi za Magharibi, huku akizilaani nchi hizo kwa madai yao bandia kuhusu suala la haki za binadamu.

Hujjatul Islam Walmuslimin Gholam-Hossein Mohseni-Eje'i alisema hayo jana Jumatano katika mkutano uliofanyika hapa Tehran na kuhudhuriwa na maafisa wa ngazi za juu wa Iran kama vile Hossein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran, Ali Shamkhani na Kazem Gharibabadi, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Haki za Binadamu Iran.

Mohseni-Eje'i amesema nchi za Magharibi ambazo zimetenda jinai za kutisha zaidi, kukanyaga haki za binadamu, kuwafurusha kwenye makazi yao watu madhulumu kote duniani, na kuharibu miundomsingi ya nchi mbalimbali, hii leo zinadai kuwa ni watetezi wa haki za binadamu.

Amebainisha kuwa, Marekani ambayo ni muungaji mkono mkubwa zaidi wa ugaidi duniani, inaituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa inaunga mkono ugaidi pasi na kutoa ushahidi wowote.

Kazem Gharibabadi, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Haki za Binadamu Iran

Kadhalika Mkuu wa Idara ya Mahakama ya Iran amesema Canada ambayo imeua raia wa asili wa nchi hiyo wakiwemo watoto wadogo, imekuwa ikiunga mkono maazimio ya kulaani eti hali ya haki za binadamu nchini Iran; kwa kutegemea madai bandia ambayo hayana msingi wowote.

Kwa upande wake, Kazem Gharibabadi, Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Haki za Binadamu Iran ambaye pia ni Mkuu wa Masuala ya Kimataifa katika Idara ya Mahakama ya Iran amesema Marekani na Wamagharibi wameligeuza suala la haki za binadamu kama mradi dhidi ya Iran, na wanatumia njia zote kuusukuma mbele mradi huo.

Tags