Jan 11, 2022 14:16 UTC
  • Brigedia Jenerali Shekarchi: Marekani ni mfadhili mkuu wa ugaidi, chanzo cha ukosefu wa usalama duniani kote

Msemaji wa Jeshi la Iran ameitaja Marekani kuwa nchi inayoongoza kwa kufadhili ugaidi duniani na kusema Washington ndiyo chanzo cha ukosefu wa usalama kote duniani.

Akizungumza katika mji wa Kerman Jumanne ya leo, Brigedia Jenerali Abolfazl Shekarchi amesema utawala wa kihalifu na mtendajinai wa Marekani uliweka wazi sura yake halisi mbele ya walimwengu kwa mauaji yake ya kigaidi dhidi ya kamanda mkuu wa kupambana na ugaidi Jenerali Qasem Soleimani.

Brigedia Jenerali Shekarchi amesema: Marekani ndiyo nchi inayoongoza duniani katika kulea ugaidi na kupora mali za watu na wanaokandamizwa." Ameongeza kuwa "Marekani inahusika na ukosefu wa usalama unaotokea duniani kote."

Vilevile ameeleza kuwa Kamanda Qasem Soleimani aliyeuawa shahidi na wanajeshi magaidi wa Marekani alisimama dhidi ya kundi la kigaidi la Daesh na kumuangamiza "mnyama huyo".

Brigedia Jenerali Abolfazl Shekarchi amesema, Marekani ndiyo aliyompa silaha na kumuunga mkono mnyama huyo mla watu na kuongeza kuwa: "Tunapaswa kuwa waangalifu tusichanganye mhanga na katili muuaji."

Amesisitiza kuwa adui ameteseka zaidi kutokana na kuuawa shahidi kwa Jenerali Soleimani ikilinganishwa na alipokuwa hai akiongoza harakati ya mapambano, akiashiria kuongezeka kwa mashinikizo ya umma yanayotaka kufukuzwa wanajeshi wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi.

Luteni Jenerali Qasem Soleimani

Shahidi Soleimani ambaye Januari 3 mwaka 2020 alielekea Iraq kwa mwaliko rasmi wa viongozi wa nchi hiyo aliuliwa shahidi akiwa pamoja na Abu Mahdi al Muhandis, Naibu Mkuu wa Kikosi cha Kujitolea cha Wananchi wa Iraq cha Hashd al Sha'abi na wanajihadi wengine wanane katika shambulio la kigaidi la jeshi la kigaidi la Marekani karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Baghdad. 

Hujuma hiyo ya kinyama ilitekelezwa kufuatia amri ya rais wa wakati huo wa Marekani Donald Trump, ambaye alijitokeza hadharani na kukiri waziwazi kuhusika na jinai hiyo, ambayo ni mfano wa wazi wa ugaidi wa kiserikali wa Washington.

Januari 8 mwaka 2020, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu lilichukua hatua ya kulipiza kisasi kwa kuvurumisha makombora kadhaa dhidi ya kambi ya wanajeshi wa Marekani ya Ain al Assad nchin Iraq na kuisawazisha kabisa na ardhi. 

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza kuwa bado haijamaliza kulipiza kisasi cha mauaji ya Shahidi Soleimani.

Tags