Jan 15, 2022 03:33 UTC
  • Abdollahian: Utekelezaji wa mkataba wa miaka 25 wa mashirikiano ya kistratejia ya Iran na China umeanza

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametangaza mwishoni mwa safari yake nchini China hapo jana: "katika safari hii, pande mbili zimekubaliana kuitangaza leo (Ijumaa) kuwa siku ya kuanza utekelezaji wa makubaliano kamili ya mashirikiano ya kistratejia baina ya nchi mbili."

Baada ya mazungumzo mapana na Waziri wa Mambo ya Nje wa China Wang Yi, Hossein Amir-Abdollahian amesema: katika safari hiyo wamekubaliana watangaze kuanza utekelezaji wa mkataba wa mashirikiano kamili ya kistratejia na ya muda mrefu ya miaka 25 kati ya nchi mbili.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa "maudhui nyingine ambayo ilikuwamo kwenye ajenda ya mazungumzo ni kwamba, ili kutekeleza mkataba wa miaka 25 na maudhui zingine tofauti za kikanda na kimataifa, tulikuja na ujumbe wa maandishi wa Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa ajili ya Rais wa China."

Halikadhalika, Amir-Abdollahian amesema, walikuwa na majadiliano ya kina pia kuhusu mazungumzo ya nyuklia ya Vienna kwa ajili ya kuondolewa vikwazo; na akafafanua kwamba, mwakilishi wa China Vienna akiwa pamoja na mwakilishi wa Russia wanatoa mchango chanya katika kuunga mkono haki za nyuklia za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kuondolewa kwa vikwazo.

Hossein Amir-Abdollahian (kushoto) na Wang Yi

Aidha amesisitiza: "matumaini yetu ni kwamba pande za Magharibi nazo pia zitaendeleza mazungumzo ya Vienna kwa mtazamo unaozingatia uhalisia wa mambo na kwa lengo la kufikia mwafaka mzuri utakaohakikisha haki na maslahi ya Iran yanazingatiwa.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amemalizia kwa kueleza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu inakaribisha kufikiwa makubaliano mazuri kwa kutumia muda mfupi zaidi unaoyumkinika, lakini hilo litategemea pande za Magharibi.../