Jan 16, 2022 08:02 UTC
  • Kamanda: Usalama wa Iran ni mstari mwekundu wa vikosi vya ulinzi

Naibu Kamanda wa Kikosi cha Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Iran amesema usalama wa taifa hili ni mstari mwekundu wa vikosi vyote vya ulinzi na usalama vya Jamhuri ya Kiislamu.

Brigedia Jenerali Alireza Elhami alisema hayo jana Jumamosi alipotembelea kambi ya Jeshi la Anga la Iran mjini Tabriz, kaskazini magharibi mwa nchi na kuongeza kuwa, majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu katu hayataanzisha mzozo au makabiliano na nchi yoyote ile, lakini hayatokaa kimya iwapo usalama wa nchi hii hususan wa anga utahujumiwa.

Ameeleza bayana kuwa, "Hii leo, maadui na mashirika ya kimataifa yanafahamu vyema juu ya jambo hili; kwamba iwapo anga ya taifa hili itahujumiwa japo kidogo, Jamhuri ya Kiislamu itatoa jibu kali na la haraka."

Mfumo wa ulinzi wa anga wa Iran

Brigedia Jenerali Elhami amesisitiza kuwa, maadui kamwe hawawezi kuthubutu kuleta chokochoko katika anga ya Iran, kutokana na umoja, mshikamano na ukuruba wa Jeshi la Iran na Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).

Naibu Kamanda wa Kikosi cha Ulinzi wa Anga cha Jeshi la Iran ameongeza kuwa, vikosi vya usalama vipo macho na vinafanya kazi bega kwa bega kuhakikisha kuwa anga ya Jamhuri ya Kiislamu ipo salama muda wote.

 

Tags