Jan 17, 2022 02:37 UTC
  • Jeshi la wanamaji la Iran; mlinda usalama katika eneo la maji ya kimataifa

Kamanda wa kikosi cha wanamaji cha jeshi la Iran amesema, kulinda usalama na kuvipa msaada vyombo vya baharini na pia kuonyesha uwezo wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu sambamba na kufikisha ujumbe wa amani na urafiki, ndio malengo ya Iran ya kuwepo kijeshi kwenye eneo la maji ya kimataifa.

Admeri Shahram Irani, ameashiria malengo ya kuwepo kikosi cha wanamaji cha jeshi la Iran katika bahari za mbali zaidi na akasema: kulinda usalama wa baharini na kutangaza kwamba, kutokana na uwezo wake, hasa katika uga wa baharini, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haijiwekei mipaka ya kuwepo katika nukta yoyote ile, ndio malengo muhimu zaidi ya kuwepo kijeshi katika maeneo ya mbali zaidi.

Admeri Shahram Irani

Iran, ni nchi ambayo kijiografia iko katika sehemu nyeti na hasasi; Bahari ya Caspian iliyoko kaskazini, Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman zilizoko kusini na Langobahari la kistratejia la Hormuz, viko kwenye eneo la mamlaka ya Iran, vikiwa ni kielelezo cha sehemu nyeti mno na ya kistratejia ilipo nchi hii katika eneo la Asia Magharibi.

Karibu asilimia 90 ya biashara za Iran zinafanyika kwa kutumia njia ya bahari; na hii ni katika hali ambayo, eneo la maji ya kimataifa linakabiliwa na kitisho cha ugaidi. Hata hivyo, uwepo imara wa kikosi cha wanamaji cha Iran umeufanya ukwamishaji wa maadui usiwe na madhara makubwa kwa uchumi wa nchi.

Kuanzia muongo wa 1980, sambamba na kushamiri na kuongezeka hatari ya uharamia katika Ghuba ya Aden na Langobahari la Bab al-Mandab, kikosi cha wanamaji cha jeshi la Iran kilianza kuchukua hatua ya kutuma kundi la manowari zikiwemo za kivita na za usindikizaji katika eneo hilo na maeneo mengine. Tangu wakati huo hadi sasa, kikosi cha wanamaji cha Iran kimetoa ulinzi kwa maelfu ya meli zinazopita eneo hilo zikiwemo za Iran na za kigeni; na katika matukio kadhaa, kimepambana ana kwa ana na maharamia na hata kuzikomboa meli zilizokuwa zimetekwa na maharamia hao.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi (aliyevaa joho jeusi) akikagua kikosi cha wanamaji

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei, ametilia mkazo mara kadhaa udharura wa kuimarisha nguvu na uwezo wa vikosi vya wanamaji. Mnamo mwaka 2009, alipohutubia katika chuo cha sayansi za baharini cha Noushahr Ayatullah Khamenei alisisitiza tena juu ya nukta hiyo aliposema: "leo hii katika maeneo mengi duniani na katika nchi yetu, kikosi cha wanamaji ni kikosi cha kistratejia; kikosi cha wanamaji inapasa kitazamwe kama kikosi cha kistratejia. Pwani za kusini-mashariki ya nchi, ambazo ziko chini ya mamlaka ya kikosi cha wanamaji cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni maeneo muhimu sana na yana fursa kubwa na nyingi kwa ajili ya kuleta maendeleo; fanyeni bidii katika maeneo hayo na yapeni umuhimu. Endelezeni shughuli za vyombo vya baharini, ambapo alhamdulillah leo hii zimepigwa hatua kubwa kulinganisha na huko nyuma; yazingatieni na kuyapa umuhimu masuala ya utaalamu wa vyombo vya chini ya bahari; yapeni umuhimu masuala ya suhula na zana za ulinzi za vyombo vya baharini katika maeneo yote, hasa katika bahari za kusini." 

Kikosi cha wanamaji cha Iran, ambacho licha ya kuwa katika mazingira ya vikwazo, lakini kwa kutegemea uwezo wake wa ndani na wataalamu wa Kiirani kimeweza kuongeza nguvu na uwezo wake, ndani ya kipindi hiki cha mwaka mmoja kimeweza kuonyesha upeo wa juu wa mafanikio yake; kwani mnamo mwezi Mei 2021, kundi la 75 la manowari za kikosi cha wanamaji cha jeshi, liliweza kwa mara ya kwanza kutumia muda wa siku 133 kukata masafa ya kilomita 45,000 za njia ya bahari, ikiwa ni safari ndefu zaidi kufanywa katika historia ya Iran ya safari za baharini. Kupitia operesheni hiyo, Iran imeweza kwa mara ya kwanza kufika Bahari ya Atlantiki Kaskazini na Nusu ya Kaskazini ya dunia; na katika operesheni yake hiyo, kundi hilo la manowari likaweza kupita Bahari ya Hindi, Atlantiki Kusini na Atlantiki Kaskazini na kuzizunguka nchi 55 za dunia.

Kikosi cha wanamaji cha Jeshi la Iran

Hivi sasa, na kutokana na kusheheni anuai za vyombo vipya na vya kisasa vya majini vilivyoundwa nchini vikiwemo vya juu na vya chini ya maji, kikosi cha kistratejia cha Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kimekuwa nguvu moja kubwa ya baharini katika eneo la Ghuba ya Uajemi na kaskazini ya Bahari ya Hindi; na nguvu na uwezo huo vina taathira na mchango mkubwa katika kulinda maslahi ya taifa, malengo ya kiulinzi na kukabiliana pia na ugaidi wa baharini, sambamba na kulinda amani na usalama katika bahari mbalimbali duniani.../