Jan 17, 2022 15:07 UTC
  • Khatibzadeh: Mambo muhimu bado yamebakia katika suala la kuondolewa vikwazo Iran

Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, masuala muhimu na ya kimsingi katika mazungumzo ya nyuklia ya Vienna Austria bado yamebakia ambapo panahitajika maamuzi maalumu ya kisiasa hususan kutoka upande wa Marekani.

Saeed Khatibzadeh amesema hayo leo hapa mjini Tehran katika mkutano wake na waandishi wa habari ambapo akizungumzia mwenendo wa mazungumzo ya nyuklia ya Iran na kundi la 4+1 yanayoendelea huko Vienna Austria amesema kuwa, mambo jumla na sehemu kubwa ya nukta zenye mjadala katika mazungumzo hayo zimefikiwa makubaliano.

Amesema kuwa, Rais wa sasa wa Marekani na timu yake ya sera za kigeni na ya mazungumzo ya nyuklia wanatambua vyema kwamba, makubaliano ya nyuklia ya JCPOA yamebakia hai kwa sababu ya Iran na siyo Marekani ambayo ilijitoa katika makubaliano hayo na wakati huo ikafanya njama za kuyasambaratisha.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikisema bayana  kwamba, kufikia mapatano mazuri ni jambo linalowezekana katika mazungumzo yanayoendelea Vienna kuhusu kuondolewa Iran vikwazo lakini inasisitiza kuwa, hilo litawezekana tu iwapo upande wa Magharibi utaonyesha nia njema.

 

Duru ya nane ya mazungumzo ya Vienna, ambayo ajenda yake kuu ni kuondolewa vikwazo vya kidhalimu na visivyo vya kisheria ilivyowekewa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ilianza mwishoni mwa mwaka uliomalizika.

Marekani ambayo ilijiondoa kwenye makubaliano ya nyuklia ya JCPOA mnamo Mei mwaka 2018 iliiwekea Iran vikwazo haramu kufuatia uamuzi wake huo na kusababisha mkwamo kwenye utekelezaji wa mapatano hayo, inashiriki mazungumzo ya Vienna nchini Austria kwa njia isiyo ya moja kwa moja.

Tags