Jan 18, 2022 02:36 UTC
  • Baada ya miaka 6; hatimaye wanadiplomasia watatu wa Iran wawasili mjini Jiddah Saudia

Baada ya kupita miaka 6 ya Saudia kutoruhusu uwakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndani ya Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC, hatimaye hivi Riyadh sasa imeruhusu na tayari wanadiplomasia watatu wa Iran wamewasili mjini Jeddah kwa ajili ya kuiwakilisha Jamhuri ya Kiislamu katika jumuiya hiyo.

Shirika la habari la ISNA limeripoti habari hiyo jana Jumatatu na kusema kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdolahian aliashiria katika mazungumzo yake na waandishi wa habari aliyofanya tarehe 23 Disemba hapa mjini Tehran akiwa pamoja na Fuad Hussein, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq kwamba Saudi Arabia imekubali kuwapa visa wanadiplomasia watatu wa Iran kwa ajili ya kwenda kuiwakilisha Jamhuri ya Kiislamu katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC mjini Jeddah.

Akihojiwa hivi karibuni na televisheni ya al Jazeera ya Qatar, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema kuwa, kupewa visa wanadiplomasia hao watatu wa Iran kwenda kuiwakilisha Jamhuri ya Kiislamu katika jumuiya ya OIC mjini Jeddah Saudi Arabia ni ishara nzuri ya kuboreka uhusiano baina ya Tehran na Riyadh.

 

Ripoti hiyo imeongeza kuwa, tayari wanadiplomasia watatu wa Iran wako kwenye ofisi za Jamhuri ya Kiislamu mjini Jeddah kwa ajili ya kuiwakilishi Tehran katika jumuiya ya OIC.

Jumuiya ya Ushikiano wa Kiislamu OIC ni chombo cha pili kwa ukubwa cha kimataifa baada ya Umoja wa Mataifa. OIC ina wanachama 57 kutoka mabara tofauti ya dunia.

Moja ya malengo ya jumuiya ya OIC ni kulinda maslahi ya Umma wa Kiislamu na kupigania amani kimataifa na ushirikiano baina ya mataifa tofauti duniani.

Tags