Jan 18, 2022 13:39 UTC
  • Admirali Sayyari: Iran hivi sasa imo katika kuvuka kipindi kigumu cha vikwazo

Naibu Mkuu wa Uratibu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, taifa la Iran hivi sasa limo katika kuvuka kipindi cha vikwazo vigumu zaidi na vya kidhalimu zaidi katika historia yake ya kimataifa.

Shirika la habari la IRNA  limemnukuu Admmirali Habibullah Sayyari akisema hayo wakati alipozungumza na wambata wa kijeshi wa nchi mbalimbali waliopo hapa Iran na kuongeza kuwa, ijapokuwa Jamhuri ya Kiislamu bado ina matatizo ya kuimarisha uhusiano wake na majirani zake kutokana na vikwazo vya kidhulma ilivyowekewa, lakini anaamini kwamba matatizo hayo yataweza kutatuliwa kwa busara na mazungumzo baina ya nchi za eneo hili bila ya kuhitajia msaada wa madola ajinabi.

Vile vile amesema, wambata wa kijeshi wa nchi za kigeni waliopo hapa nchini wana nafasi muhimu sana ya kustawisha na kuimarisha uhusiano wa pande zote baina ya nchi za ukanda huu na kuongeza kuwa, iwapo ushirikiano baina ya nchi jirani utaimarishwa, bila ya shaka yoyote manufaa makuu ya kiuchumi yatapatikana katika eneo hili zima la Asia Magharibi.

 

Naibu huyo wa Mkuu wa Uratibu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema pia kuwa, Jamhuri ya Kiislamu daima iko pamoja na wananchi wa eneo hili na haijawahi kukanyaga haki zao na inaheshimu pia uhusu wa nchi za duniani na hizo ni siasa kuu za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika muda wote.

Katibu wambata 35 wa kijeshi wa nchi mbalimbali duniani wameshiriki kwenye mazungumzo hayo yaliyojadili masuala ya usalama wa ukanda wa Asia Magharibi na mustakbali wa Afghanistan.