Jan 19, 2022 03:28 UTC
  • Rais Raisi wa Iran kutembelea Russia leo, kukutana na Rais Putin

Rais Ebrahim Raisi wa Iran leo anaelekea Russia kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Vladimir Putin wa nchi hiyo kuhusu masuala muhimu ya kieneo, kimataifa na ya pande mbili.

Ikulu ya Rais wa Russia, Kremlin, imesema akiwa mjini Moscow, Rais wa Iran atazungumza na Putin kuhusu utekelezaji wa mapatano ya nyuklia ya JCPOA.

Viongozi hao wawili pia watabadilishana mawazo kuhusu uhusiano wa pande mbili hasa kuhusu miradi ya pamoja ya kiuchumi na kibiashara.

Halikadhalika Rais wa Iran anatazamiwa kuhutubia kikao cha Bunge la Russia, Duma, na kisha atakutana na Wairani waishio Russia katika safari hiyo ya siku mbili.

Hivi sasa Iran na Russia ziko chini ya vikwazo vya kidhalimu vya madola ya Magharibi na ili kukabiliana na adui huyo wa pamoja zimeimarisha zaidi uhusiano wa kisiasa, kiusalama, kijeshi, kiuchumi na kinishati.

Nchi hizi mbili pia zinatekeleza miradi ya pamoja katika sekta za mafuta, gesi, nyuklia na reli.

Aidha Iran na Russia ziko mbioni kufanyia marekebisho mapatano ya muda mrefu ya ushirikiano yaliyotiwa saini miaka 20 iliyopita.

Tags