Jan 19, 2022 08:31 UTC
  • Kuanza utekelezaji wa mkataba wa miaka 25 wa ushirikiano wa kistratejia wa Iran na China

Hussein Amir-Abdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alitangaza mwishoni mwa safari yake nchini China hivi karibuni kwamba: "katika safari hiyo, pande mbili zimekubaliana kuitangaza Ijumaa iliyopita kuwa siku ya kuanza utekelezaji wa makubaliano kamili ya mashirikiano ya kistratejia baina ya nchi mbili."

Akibainisha umuhimu wa makubaliano hayo, Ali Shamkhani, Katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa twitter kwamba: Kuanza kutekelezwa makubaliano kamili ya ushirikiano wa kistratejia baina ya Iran na China likiwa taifa la pili kwa uchumi mkubwa duniani tena katika mazingira ambayo Marekani ingali inaendeleza  hatua zake za upande mmoja na kudumisha mashinikizo ya kiwango cha juu kabisa ikifuatilia suala la kuinyima Iran haki ya kuwa na ushirikiano wa kiuchumi na dunia, kwa hakika hili linahesabiwa na Tehran kuwa ni mafanikio ya kistratejia.

Ushirikiano wa muda mrefu kwa mtazamo wa nadharia za kiuchumi ni jambo linaloandaa uwanja wa kupanuliwa ushirikiano katika nyanja mbalimbali na wakati huo huo kusaidia kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi ambao utaleta uwiano katika ushirikiano wa kisiasa.

Kiwango hiki cha uhusiano kina malengo ya kistratejia ambacho kinaweza  pamoja na mambo mengine kudhamini ushirikiano katika nyuga nyingine kama za usalama na wakati huo huo kudhamini maslahi ya pande mbilii na ya pande kadhaa.

Muhammad Javad Zarif Waziri wa zamani wa Mashhauri yay Kigeni wa Iran akitiliana saini na mwenzake wa China hati ya ushirikiano wa miaka 25

 

Kwa mtazamo huo, ushirikiano wa miaka 25 wa Iran na China ni mwendelezo wa ushirikiano wa pande kadhaa katika fremu ya ushirikiano wa nchi za Asia. Kama ambavyo, kabla ya hapo hati ya uanachama wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Jumuiya ya Shanghai iliidhinishwa katika mji mkuu wa Tajikistan Dushanbe kwa kuhudhuriwa na Rais Ibrahim Raisi. Uanachama huu wa kistratejia una taathira muhimu pia katika mwenendo wa ushirikiano wa pande kadhaa wa Iran katika fremu ya siasa za ujirani na Asia na Tehran inaweza kunufaika na nafasi hii katika uga wa kiuchumi na kisasa.

Fauka ya hayo, China kwa upande wake nayo ni mwanachama muhimu katika Jumuiya ya Ushirikiano ya Shanghai. Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliashiria Februari 2015 katika mazungumzo yake hapa mjini Tehran na Rais Xi Jinping wa China kuhusu siasa za kibeberu za baadhi ya mataifa hususan Marekani na ushirikiano wao usio wa dhati wala ukweli na mataifa mengine na kusisitiza kwamba: Hali hii imeyafanya mataifa yasiyokubali kuburuzwa yafuatilie ushirikiano zaidi baina yao na makubaliano ya Iran na China ambayo ni kwa ajili ya uhusiano wa kistratejia wa miaka 25 nao unatathminiwa katika fremu hii ambapop kuna ulazima wa kuweko ufuatiliaji wa dhati wa pande mbili kuhakikisha kwamba, makubaliano haya yanafikia hatua ya utekelezwaji kivitendo.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Sayyid Ali Khamenei akiwa katika mazungumzo na Rais wa China Xi Jinping (mwaka 2015)

 

Kwa kuzingatia vigezo hivi, tunaweza kusema kuwa, kuanza utekelezwaji wa mkataba wa miaka 25 wa ushirikiano wa kistratejia wa Iran na China kunabeba jumbe mbili zinazoeleweka wazi na bayana.

Mosi; wigo wa uhusiano wa kisiasa na kiuchumi wa Iran ni mpana mno na Marekani haina ubavu kama inavyodai yenyewe wa kuibana na kuiweka katika mzingiro Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Ujumbe wa pili; ni sisitizo juu ya kuchanua na kustawi diplomasia ya kieneo ya Iran katika serikali ya Awamu ya 13 lakini wakati huo huo kulindwa maslahi na kuweko hali ya kuheshimiana pande mbili baina ya mataifa yenye msimamo na ambayo hayako tayari kuburuzwa.

Ushirikiano kama huu na upeo wa mbali baina ya Iran na China unadhamini malengo ya kistratejia na kuinua kiwango cha uhusiano baina ya nchi mbili. Hapana shaka kuwa, uhusiano huu unaweza kuleta mabadiliko mapya katika uhusiano wa pande mbili na wakati huo huo kuundwa kambi zenye nguvu za kisiasa, kiucumi na kiutamaduni barani Asia.